Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Diwani Athumani Msuya wakati alipohani msiba wa Biswad Msuya, Kaka Mkubwa wa Mkurugenzi huyo, nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam, Agosti 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole familia ya marehemu Biswad Msuya, Kaka Mkubwa wa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Diwani Athumani Msuya (kushoto) nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam, Agosti 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
******************************
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa kimeacha pengo serikalini na Bungeni kwani marehemu alikuwa mchapakazi, mwadilifu na mtulivu katika utendaji kazi wake
Amesema hayo leo Jumatano (Agosti 4, 2021) alipokwenda nyumbani kwa marehemu Kwandikwa, Kibaha Picha ya Ndege mkoani Pwani kutoa pole kwa familia.
“Mchango wake wa utendaji katika serikali na Bunge ni mkubwa sana alifanikiwa kuwavutia wengi kwa tabia yake ya upole, unyenyekevu na uzingatiaji wa taratibu na sheria za utumishi kila alipopangiwa kufanya kazi hivyo kifo chake ni pigo kwa taifa”
Mheshimiwa Majaliwa ameishukuru familia kwa kuridhia maombi ya kutaka mazishi yafanyike Jumatatu ijayo ili kuwapa nafasi waombolezaji wakiwemo wabunge kupata nafasi ya kusafiri kutoka waliko na kushiriki katika kutoa heshima za mwisho na mazishi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu leo amekwenda nyumbani kwa marehemu Biswad Msuya, Kaka Mkubwa wa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa kutoa pole kwa familia kufuatia kifo cha mpendwa wao.
Akizungumza na wafiwa na waombolezaji katika msiba huo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amepokea taarifa ya kifo cha marehemu Biswad kwa mshtuko mkubwa na amewataka waombolezeji wamuombee mke wa marehemu na familia ili awape utulivu na uvumilivu wakati huu wa majonzi.