……………………………………………
Adeladius Makwega, (WHUSM)-Dodoma.
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha kubwa la Ngoma za asili linalofahamika kama Tamasha la Cigogo litakalo fanyika Julai 24 na 25, 2021 katika viwanja vya Kituo cha Sanaa Chamwino Ikulu Jijini Dodoma
Akizungumza na Vyombo vya Habari Julai 22, 2021 Jijini Dodoma Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa Mfaume Said amesema kuwa tamasha hilo linaandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikishirikiana na Kituo cha Sanaa Chamwino Mkoani Dodoma na litakuwa la kukata na shoka –nguo kuchanika, ambapo amewasihi wakaazi wa Dodoma na viunga vyake kujitokeza kwa wingi.
“Hili ni tamasha linalowakutanisha wasanii wa ngoma za asili zaidi ya 600 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania tuna imani litakuwa ni fursa kubwa kwa wapenzi wa ngoma za asili kupata burudani ambayo haijawahi kutokea” amesema Mkurugenzi huyo.
Tunatambua na halina ubishi kuwa kwa muda mrefu Watanzania tumekuwa tukitilia mkazo Sanaa ya muziki wa dansi, muziki wa nje na bongo fleva tu lakini muziki wa kitamaduni umekuwa kando mathalani, muziki huu umekuwa haurudiwi kwa wingi na kuchezwa katika vyombo vya habari kama vile luninga na redio.
Bw. Mfaume amesema kufanyika kwa tamasha hilo la muziki wa wagogo litaibua ari ya kuikuza zaidi Sanaa ya ngoma za asili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kituo cha Sanaa Chamwino ,Dkt Kedomn Mapana amesema kuwa wao kama kituo wamekuwa wakiandaa matamasha ya namna hiyo kwa kipindi cha mika 16 sasa na tamasha la mwaka huu litakuwa la 12 likiwa na kauli mbiu “Utamaduni wetu Maendeleo yetu”.
“Tumemualika Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Deograthias Ndejembi katika ufunguzi akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Hassan Abbas na litahitimishwa na Waziri wa Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema Dkt Mapana.
Akizungumzia Tamasha hilo Mkuu wa Mtaa wa Talama Chamwino Ikulu, ndugu Andason Makolokolo amesema kuwa sasa Dodoma imekuwa jiji na kumekuwa na muingiliano wa makabila mengi lakini jumamosi na jumapili itakuwa wasaa wa Wagogo kuonyesha utamaduni wao kwa vitendo.
“Digule ndina mwenda, ulambi nani kadigulila ulambi. Digule dina shati, ulambi nani kadigulila ulambi” aliimba Mkuu huyo wa mtaa wa Talama.
Ndugu Makolokoli alifafanua kuwa hiyo ni sehemu tu ya wimbo wa Kigogo akisema panya ana nguo nani amemnunulia huo ni uwongo, panya ana shati, huo uwongo nani kamnunulia. Akisema wimbo huo unaimbwa na wagogo mara baada ya mavuno kusherekea furaha ya mavuno.
Kituo cha Sanaa Chamwino kwa muda mrefu kimekuwa ni miongoni mwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kwa karibu na serikali kwa kukuza sanaa na utamadauni wa Mtanzania ambapo kilisajiliwa kwa mujibu wa Sheria Nambari 23 ya mwaka 1984 ya Baraza la Sanaa la Taifa BASATA.