Mkuu wa Wilaya ya Iramba Selemani Mwenda, akizungumza baada ya kukabidhiwa Mwenge wa Uhuru. |
Na Dotto Mwaibale, Iramba Singida.
SERIKALI Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na wananchi mapema leo asubuhi wameupokea Mwenge wa Uhuru ukitokea mkoani Tabora.
Miradi yenye thamani ya Sh. 8,182,219,653.99 inatarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru 2021, mkoani hapa ambao mbio zake zimeanza katika Wilaya ya Iramba.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa Mwenge huo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk.Balozi Batilda Buriani katika Kijiji cha Mseko wilayani Iramba Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge alisema Mwenge huo utakimbizwa kwa muda wa siku tano katika wilaya tano kwa kuanzia na Wilaya ya Iramba na utahitimisha mbio zake Julai 24/2021 ambapo utakabidhiwa Mkoa wa Dodoma.
Alisema Mwenge wa Uhuru utakapokuwa Mkoani hapa utakimbizwa jumla ya kilometa 642.3, utapitia jumla ya miradi 55 inayohusu TEHAMA, Elimu, Afya, Mazingira, Maji, Biashara, Barabara na Programu za Rushwa, Malaria, mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya,VVU/UKIMWI na Lishe.Miradi 9 itazinduliwa, miradi 2 itafanyiwa ufunguzi, miradi 6 itawekwa jiwe la msingi, miradi 36 itakaguliwa na Miradi 2 itatembelewa.
Alisema miradi yote itakayopitiwa na mwenge huo itakuwa na thamani ya Sh. 8,182,219,653.99 ambapo alitoa mchanganuo wake kuwa nguvu za wananchi ni Sh. 1,957,623,652.58, Halmashauri Sh. 69,630,194.42, Serikali Kuu Sh.4,627,922,247.27 na Wahisani sh.1,527,043,559.72.
Alisema ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka2021 ambao utatolewa maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkoa wa Singida ni “Matumizi Sahihi ya TEHAMA” chini ya Kauli Mbiu inayosema TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu;Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji.
Dk. Mahenge alisema Mkoa wa Singida umekuwa ukiamini kuwa TEHAMA ni msingi wa maendeleo endelevu, kwani matumizi sahihi ya miundombinu na mifumo ya TEHAMA yamewezesha kurahisisha mawasiliano, ukusanyaji na kuongeza mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya Fedha za Umma, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika kuwatumikia Wananchi, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,kurahisisha taratibu za manunuzi ya Umma na kuondoa mianya ya rushwa na ubadhilifu, urahisi kwa wananchi kulipia ankara mbalimbali, kurahisisha na kuwezesha upatikanaji wa Takwimu mbalimbali kwa usahihi na kwa wakati.
” Kwa kutambua faida hizi zitokanazo na matumizi sahihi ya TEHAMA, Mkoa wa Singida umeendelea kusimamia mifumo ya TEHAMA zaidi ya 30 inayotumika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti ya Mkoa pamoja na Taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya Mkoa wa Singida,” Mahenge.
Alitaja baadhi ya Mifumo ya TEHAMA inayotumika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine ni pamoja na mifumo ya fedha ya ukusanyaji wa mapato na matumizi ambayo ni ‘Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS)’, ‘e-Revenue Management System’ unaotumiwa na TARURA. Mifumo ya uhasibu Serikalini (MUSE)naFFARS.
Aidha Dk. Mahenge alitaja mfumo mwingine kuwa ni wa TEHAMA wa TANEPs unahusika na Manunuzi ya Umma, Mfumo GoTHOMIS unatumika kudhibiti makusanyo ya vituo vya kutolea huduma za Afya pamoja na upotevu wa dawa na vifaa tiba, mfumo waTEHAMA wa ukusanyaji wa takwimu za Kilimo (ARDS), mifumoya PREM, PREMs, School Information System (SIS) na Annual School Sensor (ASC) kwaajili ya kupata takwimu sahihi za elimu na mfumo wa (HCMIS)) kwaajili ya Taarifa za kiutumishi na Mishahara.