Home Mchanganyiko MAJALIWA: TUMEDHAMIRIA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BANDARI

MAJALIWA: TUMEDHAMIRIA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BANDARI

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa  Bandari kwenye kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa  Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam, Julai 20, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  Eric Hamissi akizungumza katika  kikao kazi cha wadau wa Bandari kilichoitishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,  katika  ukumbi wa Ofisi Ndogo  ya Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam, Julai 20,  2021.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC),  Masanja Kadogosa wakati alipozungumza  katika  kikao kazi cha wadau wa Bandari kilichofanyika  kwenye   ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam, Julai 20, 2021.Wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Eric Hamissi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*****************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya bandari ili kuvutia idadi kubwa ya watumiaji zikiwemo nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 20, 2021) alipokutana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, Mkurugenzi wa Bandari, TASAC, TBS, TMDA, Kamishna wa Forodha pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya usafirishaji.

Amesema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika uboreshwaji wa huduma mbalimbali bandarini zikiwemo za upakuaji wa mizigo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mizigo yote inayopitia bandarini inapakuliwa katika kipindi cha muda mfupi.

Amesema bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zimefanyiwa maboresho makubwa, hivyo amewasisitiza wadau wa sekta binafsi waendelee kuleta meli za kutosha.

Waziri Mkuu amesema mbali na maboresho yaliyofanyika katika bandari hizo, pia bandari za Kabwe, Kasanga nazo zimeboreshwa pamoja na ujenzi wa bandari ya Karema ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria katika nchi za Congo, Zambia na Burundi.

Naye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Chamuriho amesema kuwa ujenzi ndani ya bandari ya Dar es Salaama unaelekeka kukamilika “Gati zote saba tumezimaliza na sasa tunamalizia eneo la makontena katika gati namba sita na saba ambalo litakamilika mwezi Agosti, 2021, hii itasaidia kuongeza ufanisi ndani ya bandari”

Pia ameongeza kuwa wataendelea kuzingatia masuala yote ya kisheria, kisera, kiutawala na kiutendaji na kuyasimamia kikamilifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa bandari ili kila anayeitumia aweze kunufaika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Msanja Kadogosa amesema kuwa Shirika hilo limefanikiwa kukarabati mabehewa zaidi ya 200 ya mizigo ambayo yanaenda nchi za Burundi na Kongo.

Kadogosa ameongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha, Serikali imelitengea Shirika hilo bajeti kwa ajili ya kukarabiti mabehewa 660 na kazi ya ukarabati itaanza muda wowote, pia vichwa vingine tisa vitakarabtiwa kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa mizigo.

Akizungumzia kuhusu usafirishaji wa mafuta nchini Uganda, Kadogosa amesema kuwa wameanza kutekeleza zoezi hilo ambalo lilikwama kwa takribani miaka 15 na wiki ijayo watapeleka lita milioni moja kwenda nchini Uganda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa sekta ya bandari wameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kuboresha sekta hiyo na wameshauri hatua zaidi zichukuliwe ili kuvutia zaidi watumiaji wa bandari nchini.