Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Tume ya Utumishi wa Umma) Bw.Richard Cheyo akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha mkutano wa nne wa mwaka fedha 2020/2021.
Katibu Msaidizi (Idara ya Rufaa na Malalamiko) Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Peleleja Masesa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha mkutano wa nne wa mwaka fedha 2020/2021.
****************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM.
Tume ya Utumishi wa Umma imepokea na kutolea uamuzi rufaa 107 na malalamiko 08 yaliyowasilishwa na watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na mamlka zao za ajira na mamlaka za nidhamu.
Ameyasema hayo leo Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Tume ya Utumishi wa Umma) Bw.Richard Cheyo leo Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha mkutano wa nne wa mwaka fedha 2020/2021.
Akizungumza na waandishi wa habari Bw.Cheyo amesema Tume ilijadili na kutoa uamuzi wa rufaa 107, ambapo rufaa 76 zilikataliwa, rufaa 09 zilikubaliwa bila masharti na rufaa 12 zilikubaliwa kwa masharti kuwa mashauri hayo yaanzishwe upya kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Aidha Bw.Cheyo amesema kuwa rufaa 10 zilikatwa nje ya muda hivyo zilitupiliwa mbali na tume.
“Tume ilipokea na kutolea uamuzi malalamiko 08 kati ya hayo malalamiko 03 yalikataliwa. Malalamiko 05 yalikubaliwa bila masharti”. Amesema Bw.Cheyo.
Amesema Tume katika kushughulikia na kutoa uamuzi wa rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa mbele yake, ilibaini kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongoni mwa watumishi wa Umma, na baadhi ya waajiri, mamlaka za ajira na mMamlaka za Nidhamu.
Pamoja na hayo Bw.Cheyo amesema Watumishi wa Umma,Waajiri, mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu wanapaswa wakati wote kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria,kanuni.Taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali.
Hata hivyo amesema kamati za Uchunguzi zinazoundwa na Mamlaka za Nidhamu kuchunguza tuhuma wanazokabiliwa nazo watumishi wa umma zinatakiwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Amesema Waajiri wanatakiwa kushughulikia masuala ya kinidhamu ya watumishi wanaotuhumiwa kufanya makosa kwa wakati ili hatua stahiki zichukuliwe na ikithibitika kuwa hawana makosa wastaafu kwa heshima.
Amesisitiza kuwa Watumishi wote wa Umma wanapaswa kuzingatia Kanuni za Maadili katika Utumishi wao na kutoa huduma bora kwa wananchi.