Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo June 29,2021 jijini Dodoma.
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Shaka Hamdu Shaka akizungumza na waandishi wa habari kuhusu yaliyojadiliwa kwenye kikao cha kawaida cha NEC kilichofanyika leo June 29,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………………………
KIKAO cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa(NEC) kimefanyika Jumanne leo Juni 29, 2021 chini ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa White House Dodoma.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wameazimia na kutoa tamko la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Husein Ali Mwinyi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuiongoza nchi na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2020 – 2025.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Juni 29,2021 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Shaka Hamdu Shaka amesema aidha wajumbe hao wamebainisha kuwa tokea nchi ilipopata msiba mkubwa wa kuondokewa na aliyekuwa Rais, Hayati Dkt. John Magufuli, ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa na kuonyesha dira ya serikali anayoiongoza kuwa inazingatia uadilifu, Utawala wa Sheria, Haki, Usawa, kuimarisha misingi ya demokrasia, umoja na mshikamano zaidi kuendelea kutunza Amani na usalama wa nchi.
Pia katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesisitiza juu ya azma ya Serikali inayoiyongoza kuhakikisha inakamilisha na kuiratibu vyema miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa na inayoendelea kutekelezwa sambamba na kuhakisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi.
“Miradi yote iliyopo kwenye maeneo yenu viongozi wa CCM mnao wajibu wa kuifatilia, kuikagua na kujua uendelevu wake bila uwoga kwani huo ni wajibu wenu wa msingi katika kutusimamia Serikali, hilo liende sambamba na kuhakikisha mnasaidia kuona mapato ya Serikali hayapotei.
“Katika vyanzo vyote vya ukusanyaji, ikumbukwe ninyi ndio kioo cha kutumurika, kwavile ilani inayotekelezwa ni ya Chama Cha Mapinduzi lazima ifanikiwe kwa kiwango kikubwa” Ndugu Samia Suluhu Hasasan Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.