Home Mchanganyiko WMA WAADHIMISHA KILELE CHA SIKU YA VIPIMO DUNIANI KWA KUTEMBELEA NA KUHAKIKI...

WMA WAADHIMISHA KILELE CHA SIKU YA VIPIMO DUNIANI KWA KUTEMBELEA NA KUHAKIKI SEHEMU ZA KUFANYIA MAZOEZI (GYM)

0

Mkurugenzi Mkuu wa gym ya Herros Gym Fitness Bw. Khalid Faraji akitoa maelezo kwa maafisa wa Wakala wa Vipimo WMA mara baada ya maafisa hao kutembelea gym hiyo kuhakiki vipimo ikiwa leo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vipimo  Duniani.

Mteja akipima uzito kabla hajaingia katika chumba cha kufanyia mazoezi ya viungo.

Wateja wakifanya mazoezi katika gym ya Herros Gym Fitness Jijini Dar es Salaam.

Maafisa wa Wakala wa Vipimo wakishuhudia namna ya ufanyaji mazoezi katika Gym ya Herros Gym Fitness leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea gym hiyo kuhakiki vipimo ikiwa leo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vipimo  Duniani.

mwalimu wa gym ya Herros gym fitness Bw.Eddo Hassan akiwaonesha maafisa wa Wakala wa Vipimo (WMA) namna wateja wanapofika eneo hilo na kufanya mazoezi mara baada ya  maafisa hao kutembelea gym hiyo kuhakiki vipimo ikiwa leo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vipimo  Duniani.

*************************

NA EMMANUEL MBATILO

Siku ya leo Mei 20 ambapo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani , Wakala wa Vipimo (WMA) wametembelea sehemu ya kufanyia mazoezi (Gym) katika wilaya ya Kinondoni kuhakiki vipimo katika chuma za kufanyia mazoezi.

Akizungumza mara baada ya kufanya uhakiki katika maeneo hayo Kaimu Meneja WMA mkoa wa Kinondoni Bw.Charles Mavunde amesema wamekuwa wakivihakiki vyuma vya kufanyia mazoezi kwasababu kuyanyua vyuma ambavyo  aidha vinauzito mkubwa ama kunyanyua vyuma upande mmoja mdogo na  upande mwingine mkubwa kuna uwezekano mkubwa kuleta athari kwa mtumiaji.

“Kila mwaka tumekuwa tukipita katika  gym mbalimbali ambazo zipo  maeneo yetu kuhakikisha kwamba vile vyuma wanavyovinyanyua vinakuwa uzito uliosahihi na hatimae tunawapa vyeti”. Amesema Bw.Mavunde.

Aidha Bw.Mavunde ametoa wito kwa wamiliki wa gym nawananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba wanatumia vyuma ambavyo vinauzito uliosahihi na kuruhusiwa kisheria.

Pamoja na hayo ametoa rai kwa wamiliki wa gym ambao mpaka  sasa wanatoa mazoezi kwa wananchi kwa kutumia vyuma ambavyo  havijahakikiwa na Wakala wa Vipimo  wahakikishe kwamba wanakutana na wakala hao  ili  kuhakikisha wananchi  wanapata mazoezi katika vipimo vinavyokubalika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa gym ya Herros Gym Fitness Bw. Khalid Faraji amesema mashine zote za kufanyia  mazoezi zipo sawa na hakuna malalamiko kutoka kwa wateja wao  wanaofika  hapo  kwaajili ya kufanya mazoezi hivyo ni kutokana na wao kushirikiana na wakala wa vipimo kuhakiki vyuma vya kufanyia mazoezi kila mara.

Nae mwalimu wa gym ya Herros gym fitness Bw.Eddo Hassan amesema kuwa wale ambao wanafanya mazoezi mtaani wanaweza kupata athari mbalimbali ikiwemo kulemaa upande mmoja zaidi  ya kwingine.