Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  wakiwa katika picha ya pamoja  na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa mara baada ya ufunguzi wa Mafunzo ya Wiki Moja ya Kuwajengea uwezo, maarifa na ustadi katika masuala ya Mikataba. Mafunzo hayo yanafanyika Jijini Dodoma na yameratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na  Chama cha Wahandisi Elekezi (ACET). Mkufunzi Mkuu wa Mafunzo haya ni Mdahisi Marco Benedict Kapinga anayetambuliwa na FIDIC kama Mkufunzi 

…………………………………………………………………………………..

Na Mwandishi Maalum

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa amesema, mafunzo   wanayopewa   Mawakili  wa Serikali wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, siyo tu yatawajengea uwezo na maarifa zaidi  katika utekelezaji wa majukumu yao, bali pia yatawawezesha  kuishauri vizuri Serikali.

Dkt. Longopa ameyasema hayo leo May 3,2021 wakati akifungua kwa  niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, mafunzo  ya siku  wiki moja  kuwajengea uwezo, maarifa na utaalamu zaidi  Mawakili zaidi ya 20 wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa  Mikutano  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa  Dkt. Longopa,  katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali  watapatiwa utaalamu na nyezo za matumizi ya   Mikataba FIDIC   iliyomo katika  Kitabu Chekundu  (Conditions of Contract for Constraction) na Kitabu cha Njano. ( Conditions for Contract for Plant and Design Build)

Mikataba hii ya Kitabu Chekundu na Kitabu cha Njano hutumika pia kwenye ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo  kama  Mradi wa Kufua Umme wa  ‘Julius Nyerere Haydro- Power’ na Mradi wa Ujenzi wa  Reli ya  Kisasa ( SGR).

“Nimatumaini yangu kwamba, mtashiriki kikamilifu  katika mafunzo haya  ambayo yatawasaidia sana, siyo tu katika  kuwaongezea elimu, maarifa na ustadi katika utekelezaji wa majukumu  yenu wakati kutoa ushauri,  wakati wa  majadiliano, wakati mnapo pekua upekuzi wa mikataba au wakati wa  usimamizi wa mikataba na uuandaaji wa Sheria bali pia    yatawasaidia kutatua baadhi ya  changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yenu ya  Kila siku” akasema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha Dkt. Longopa ameeleza kuwa, mafunzo endelevu ya muda mrefu na muda mfupi kwa Mawakili wa Serikali na Kada nyinginezo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ni  ni muhimu na yanahitajika sana  kwani  licha ya kuwasaidia Mawakili lakini   yataisaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi kwa mafanikio na pia katika kuhakikisha Thamani  Halisi ya Fedha inapatika  kupitia miradi ya maendeleo ili kuwaletea wananchi  maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kwa upande wake, Mkufunzi Mkuu   wa mafunzo  hayo na anayetambuliwa na ‘ Federation of Consulting Engineers’ (FIDIC)  Mhandisi Marco Benedict Kapinga, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo  hayo, amesisitiza kwamba, mafunzo hayo yatawawezesha Mawakili wa Serikali  pamoja na mambo mengine namna ya kulinda maslahi ya Taifa lakini pia yanawajengea uwezo na wao wakuja kuwa wakufunzi kwa mawakili wengine.

Kama sehemu ya mafunzo Mawakili hao watapata fursa ya kuutembelea mradi wa SGR kama sehemu ya kupata uelewa zaidi.

Mawakili hao wanatoka katika Idara ya Mikataba na Makubaliano,  Idara ya Uandishi wa Sheria, Idara ya  Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria na Kitengo cha Manunuzi.