Home Uncategorized RAIS KENYATTA:TUMEMPOTEZA MWANAMAGEUZI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

RAIS KENYATTA:TUMEMPOTEZA MWANAMAGEUZI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

0
Rais wa Kenya Mhe.Uhuru Kenyatta,akihutubia wakati  wa kutoa salamu za rambirambi kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli hafla ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kitaifa imefanyika uwanja wa Jamhuri Dodoma leo Machi 22,2021.

…………………………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma


Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imempoteza mwanamageuzi na mzalendo wa kweli ambaye aliziunganisha Nchi zote zinazounda Jumuiya hiyo huku akitaka zijiendeshe zenyewe bila kutengemea kutoka kwa wafadhili.

Hayo ameyasema leo Machi 22,2021 jijini Dodoma wakati wa kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk John Magufuli, Rais Kenyatta ametoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na watanzania kwa ujumla kufuatia kifo cha Dk Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.

Rais Kenyatta amesema kwenye uongozi wa Dk Magufuli aliwafundisha wana-jumuiya ya Afrika Mashariki kujitegemea kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuacha kutegemea misaada kutoka mataifa ya Nje.

” Afrika imempoteza mwanamageuzi wa kweli, mimi binafsi nimempoteza rafiki wa kweli ambaye tulipigana simu kila siku tukishirikiana katika mambo mbalimbali ya kujenga mataifa yetu.

Kwako Dada yangu Rais Samia Suluhu Hassan barabara umeoneshwa, sisi tupo nyuma yako nikuombe uendeleze kazi kubwa iliyoanzishwa na ndugu yetu Dk John Magufuli, niwaombe watanzania muungane mumpe ushirikiano Rais Samia ili aweze kuendeleza falsafa ya Dk Magufuli ya Hapa Kazi Tu, ” Amesema Rais Kenyatta.

Amesifu jitihada kubwa zilizofanywa na Dk Magufuli katika kipindi chake cha uongozi kwa kujenga miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, ujenzi wa kisasa huku akisema mchango wake katika ukuaji wa uchumi hautofutika kwa miaka yote.

Hafla ya kumuaga Hayati Dkt.John Magufuli kitaifa imefanyika katika uwanja wa Jamhuri Dodoma na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassana pamoja na Marais wa nchi zaidi ya 10 na viongozi mbalimbali kutoka nje ya Tanzania wamehudhuria tukio la kutoa heshima za mwisho.