Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Ruvuma Addo Mwisho anayezungumza akiwa na Kamati ya Siasa ya chama hicho mkoani Ruvuma katika Hifadhi za Jumuiya za Mbarang’andu na Kimbanda Wilayani Namtumbo.
***********************************
NA SULEIMAN MSUYA, SONGEA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Ruvuma kimepongeza Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) kwa kununua mashine na Shirika la Mpingo na Mandeleo (MCDI) kujengea wananchi uwezo wa kuongeza thamani ya mazao ya misitu mkoani hapo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Ruvuma Addo Mwisho wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mashine ya kuchakata mazao ya misitu iliyonunuliwa na MCDI kwa ufadhili wa FORVAC.
FORVAC ni program inayotekelezwa chini ya Idara ya Misitu na Nyuki na kufadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland.
Mwisho amesema shughuli zinazofadhiliwa na FORVAC zimekuwa na matokeo chanya hali ambayo inarahisisha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 hadi 2025 Ibara ya 69 kigungu F.
Amesema awali miradi hiyo ilipotambulishwa baadhi ya wananchi walikataa na wengine walishangaa ila wachache walielewa na leo wanaona faida.
Mwenyekiti amesema walipita katika vijiji vya mradi na kufanikiwa kutoa elimu ambapo leo matokeo mazuri yameanza kuonekana.
“Mradi huu umepokelewa kwa changamoto ila leo tunaona matunda ambapo tumepokea mashine ya kuchakata mazao hivyo Ilani ya CCM inatekelezwa,” amesema.
Mwisho amesema CCM mkoa inaomba Serikali kuendelea kutoa elimu ili wanufaika wawe wengi zaidi hali itakayosaidia kupunguza umaskini.
Mwenyekiti amesema neema ya ardhi yenye rutuba ambayo Ruvuma imepewa inapaswa kutumika vizuri kwa uendelevu.
Amesema CCM itaendelea kuunga mkono juhudi wadau wote ambao wameamua kujitolea kusaidia huduma za kijamii, mazingira na nyingine nyingi.
“Tunapenda kuwakaribisha wadau wengine waje waungane na FORVAC na MCDI kuhakikisha dhana ya mnyororo wa thamani inaonekana kwenye mazao ya misitu,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Hamisi Abdallah amesema chama kitaunga mkono jambo lolote ambalo linachochea kubadilisha maisha ya wananchi.
“Miradi hii inachangia kuongeza kipato cha wananchi, ajira na thamani ya mazao ya misitu hivyo CCM itaendelea kuunga mkono kwani ndio lengo la Ilani yetu,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea, Benas Komba amesema ujio wa mashine hiyo itachochea uzalishaji kwenye mazao ya misitu hivyo watahakikisha ushiriki wa Serikali unakuwa wa kutosha.
Komba amesema mashine hiyo itachangia ongezeko la mapato, ajira na ukuaji wa uchumi wa wananchi, vijiji na halmashauri.