Home Mchanganyiko WAWILI JELA KITETO BAADA YA WALIYEMDHAMINI KURUKA DHAMANA

WAWILI JELA KITETO BAADA YA WALIYEMDHAMINI KURUKA DHAMANA

0

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu, akizungumza na waandishi wa habariĀ 
****************************************
Na Mwandishi wetu, Kiteto
WAKAZI wawili wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Leshoni Moita na Muunjuri Tepeno, wamehukumiwa kwenda jela miezi sita kila mmoja kwa kushindwa kulipa shilingi laki tano ya dhamana baada ya mtuhumiwa wa kesi ya rushwa Moita Tepeno kuruka dhamana.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Kiteto, Mossy Sasi baada ya washtakiwa hao kushindwa kulipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja, baada ya kumdhamini mtuhumiwa Tepeno kisha akatoroka.
Hakimu Sasi amesema washtakiwa hao walimdhamini Tepeno kwenye kesi ya jinai namba 22/2020 iliyopo mahakamani ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Amesema Tepeno alijipatia fedha hizo kwa udanganyifu kuwa ametumwa na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Kanali Patrick Songea ili mtu ambaye binti yake mwanafunzi alipata ujauzito asichukuliwe hatua.
Amesema baada ya Tepeno kuruka dhamana mahakama iliamuru wadhamini wakamatwe na kutakiwa kutoa fungu la dhamana sh500,000 kila mmoja na kukamatwa Machi 10 mwaka huu wakashindwa kulipa kisha wakapelekwa mahabusu.
Washtakiwa hao walirudishwa tena mahakamani Machi 16 na kutakiwa kulipa fedha za dhamana kila mmoja shilingi laki tano wakashindwa, ndipo wakahukumiwa kwenda jela miezi kila mmoja na kisha wakapelekwa gereza la wilaya ya Kiteto kuanza kifungo.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ametoa onyo kali kwa wana Manyara wote wenye mtindo wa kuwadhamini washtakiwa mahakamani na kisha kuwatorosha waache mara moja.
Makungu amesema kwa watakaoshupaza shingo zao wafahamu kwamba yatawapata kama yaliyowapata Tepeno na Leshoni kwani sheria ni msumeno hukata mbele na nyuma.