Home Mchanganyiko AFISA MTENDAJI WA KIJIJI (VEO) APONEA CHUCHUPUKU KWENDA JELA KWA RUSHWA

AFISA MTENDAJI WA KIJIJI (VEO) APONEA CHUCHUPUKU KWENDA JELA KWA RUSHWA

0
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.
…………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Kiteto
Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Ndedo Kata ya Makame Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Yusuf Mrisho amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 50.
Afisa mtendaji huyo VEO Mrisho hata hivyo alilipa faini hiyo ya shilingi milioni moja na kuepuka kifungo hicho cha miaka mitatu kwenda kutumikia kifungo jela.
Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakakama ya wilaya ya Kiteto, Mossy Sasi ametoa hukumu hiyo jana Mji mdogo wa Kibaya.
Hakimu Sasi amesema Mrisho ametiwa hatiani kwa makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa ya sh50,000 kinyume na kifungu cha 15 (1) kikisomwa na 15 (2) vya sheria ya kuzuia rushwa namba 11/2007 .
“Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka wa makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa, ambapo kwa kila kosa faini ni laki 5 au kifungo cha miaka mitatu jela,” amesema hakimu Sasi.
Hata hivyo, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema awali ofisi yao ya Kiteto ilipokea taarifa ya rushwa ya kikundi cha Upendo cha Ndedo.
Makungu amesema Mrisho aliomba rushwa ya sh50,000 kwa kikundi cha Upendo ili awaandikie barua ya kufufua akaunti yao ya benki ambayo ilikuwa imelala.
“Ofisi ya TAKUKURU Kiteto ilifanya uchunguzi wa awali na kujiridhisha juu ya tuhuma husika ambapo mtego wa rushwa uliandaliwa na mtuhumiwa kukamatwa na kufunguliwa kesi ya jinai namba 119/2019,” amesema Makungu.
Amesema TAKUKURU inawataka watumishi wote wa mkoa wa Manyara, kutoa huduma kwa weledi na uadilifu ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa.
“Wananchi wana matumaini makubwa kwao juu ya kutatuliwa changamoto mbalimbali zinazowakabili na wasitumie matatizo ya jamii kujinufaisha wao binafsi,” amesema Makungu.