Kushoto ni nyanya zilizoagizwa kufanyiwa mabadiliko ili kuwa ilivyo nyaya za kulia
**************************************
WAFANYABIASHARA, mafundi wa umeme pamoja na wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wameliomba Shirika la viwango Tanzania(TBS) kutoa ufafanuzi wa nyaya zinazopaswa kuwepo katika soko ili kuwaondolea mkanganyiko wa matumizi wa nyaya hizo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, wafanyabiashara pamoja na wananchi hao, walisema kwa namna hali ilivyo sasa ni ngumu kwao wao kutambua nyaya zipi hususani za uunganishaji wa umeme majumbani zinapaswa kuwepo madukani na nyaya zipi hazitakiwi kuwepo.
Kwa mujibu wa wananchi hao, hapo awali TBS ilitangaza kusitishwa kwa matumizi ya nyaya nyekundu na nyeusi na badala yake zitumike rangi ya blue, ‘brown’ (ugolo) na kijani kulingana na mahitaji ya soko la kimataifa.
Walisema kufuatia agizo hilo, baadhi yao waliamua kuachana na matumizi ya nyaya hizo zilizozuiliwa na kununua nyaya zenye rangi iliyopendekezwa ili kuepuka kuvunja sheria ambayo kimsingi ilitaka agizo hilo kutekelezwa.
Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyepo eneo la Karikoo Abdallah Hussein alisema cha ajabu licha ya agizo hilo kutolewa, bado nyaya hizo zenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na nyekundu zimeendelea kuuzwa katika maduka mbalimbali jambo aliloomba lifuatiliwe.
“Hii inatuchanganya sana sisi watumiaji na wafanyabiashara kwa kuwa tunajua kuendelea kutumia nyaya hizo ni sawa na kuvunja utaratibu, tunaomba suala hilo lifuatiliwe ikibidi kufanya ukaguzi katika viwanda vyote vinavyozalisha ili wahusika wabainike” alisema Hussein.
Bila kuvitaja viwanda hivyo, alisema ni wazi kuwa vinakiuka kwa makusudi agizo hilo la TBS ambayo kimsingi ndiyo chombo cha Serikali kilichopewa dhamana ya kusimamia viwango vya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa ama kuingizwa nchini.
Aidha kwa uchunguzi wao wamebaini pia zipo baadhi ya nyaya hizo ambazo zimezuiliwa matumizi huingizwa hapa nchini na moja ya kampuni hivyo kutaka uchunguzi zaidi kufanyika.
Walisema kwa sawa nyanya hizo bado zinaendelea kuuzwa katika baadhi ya maduka hususani yaliyopo mitaa ya Narung’ombe na Gogo iliyopo eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.