Home Mchanganyiko MADIWANI KALIUA WATAKIWA KUWEKA MBELE MASLAHI YA UMMA

MADIWANI KALIUA WATAKIWA KUWEKA MBELE MASLAHI YA UMMA

0

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati  akifungua jana mafunzo ya kuwajengea uwezo Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kuhusu majukumu  na mipaka yao.

Baadhi ya Madiwani na Wakuu wa Idara na Vitengo vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua wakiwa ufunguzi jana wa mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Madiwani wa Halmashauri hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Jerry Mwaga akieleza  malengo ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Madiwani wa Halmashauri hiyo wakati ufunguzi rasmi jana.
Picha na Tiganya Vincent
********************************************

NA TIGANYA VINCENT

                                                     

MADIWANI  wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua wametakiwa kuhakikisha maslahi ya umma ndio kipaumbele chao cha kwanza katika utekelezaji wa majukumu ya kwenye kipindi chote cha kuwa madarakani.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano wanatakiwa kuhakikisha wanaepuka mgongano wa maslahi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili waweze kutetetea haki za wananchi bila kuogopa na kumuonea mtu.

Dkt. Sengati alisema wanapaswa kuhakikisha wanasiamia Sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kuleta maendeleo yanayotakiwa kwa wananchi.

 “Diwani ambaye ataweka maslahi binafsi mbele atakuwa amepoteza sifa kwa wananchi ya kuchaguliwa tena …lakini Diwani atakayesimama vema katika nafasi yake na kuacha alama nzuri katika jamii , wananchi watasema huyo alikuwa Diwani wa wananchi na atakuwa na fursa ya kuchaguliwa tena” alisisitiza

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka kufahamu mambo ya kuzingatia katika uibuaji , upangaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

Dkt. Sengati aliongeza kuwa wanatakiwa kufahamu usimamizi na udhibiti wa fedha katika Halmashauri yao ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Jerry Mwaga alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Madiwani waweze kujua majukumu yao , kufahamu mipaka na madaraka yao katika kutoa maazimio kuhusu masuala ya kinidhamu kwa watumishi.

Alisema mafunzo hayo yatawawezesha Madiwani kufahamu mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na kufahamu maadili yao na mgongano wa maslahi.