Home Mchanganyiko TAASISI NNE KUCHUNGUZA SHULE YA DON BOSCO – TANGA

TAASISI NNE KUCHUNGUZA SHULE YA DON BOSCO – TANGA

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela leo Februari 22, 2021 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Waziri Ummy Mwalimu yuko Mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za utunzaji na uhifadhi wa mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Padre Thomas Kiangio leo Februari 22, 2021 mara baada ya kuwasili katika Shule ya Sekondari ya Don Bosco kukagua athari za vumbi, kelele na Moshi unaotoka katika Kiwanda cha Saruji cha Rhino jirani na Shule hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Bw. Arnold Mapinduzi Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini baada ya kuwasili katika Shule ya Sekondari ya Don Bosco kukagua athari za vumbi, kelele na Moshi shuleni hapo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy akikagua Kiwanda cha kuzalisha chokaa cha Neelkanth Chemical Limited kilichopo katika Jiji la Tanga. Wa pili kulia ni mmiliki wa Kiwanda hicho Bw. Rashid Hamoud (Liemba)

**************************************

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu amesema ataunda timu ya wataalamu kutoka Taasisi nne kuchunguza athari za vumbi linalodaiwa kuathiri wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Don-Bosco katika Jiji la Tanga.

Kauli hiyo ameitoa hii leo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa Ofisini kwake kupitia viongozi wa Shule hiyo na wakazi wa maeno jirani

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Wizara ya Viwanda pamoja na Wizara ya Afya kufanya uchunguzi wa kina na kuishauri Serikali ili iweze kutoa maamuzi sahihi.

Akiwasilisha taarifa ya athari za vumbi na kelele katika Shule hiyo Mkuu wa Shule Sr. Sebastiana Mlacha amesema kwa muda mrefu Kiwanda hicho kimekuwa kikilamikiwa kuchafua mazingira kutokana na moshi, kelele na vumbi zitokanazo na uendeshaji wa mitambo kiwandani hapo.

“Kidato cha kwanza mwaka huu tulipokea wanafunzi 150, mpaka sasa wamebaki wanafunzi 40 tu, wengine wamehama kutokana na athari za moshi, kelele na vumbi ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaathiri afya za wanafunzi hawa” Alisisitiza Sr. Mlacha.

Nae Msimamizi wa Jimbo Katoliki la Tanga, Padre Thomas Kiangio amesema ni vema wawekezaji hao wakabadili teknolojia kiwandani hapo ili kunusuru afya za wanafunzi shuleni hapo pamoja na wakazi wa eneo hilo, ambazo zinaathirika kwa kiasi kikubwa.

“Wanafunzi hawa wengi wanasumbuliwa na magonjwa ya ngozi, macho na kikohozi kutoka na moshi na vumbi, pia inakuwa vigumu kusoma nyakati za usiku hata mchana kutokana na kelele zilizokithiri kiwandani hapo.” Alisisitiza PadreThomas Kiangio.

Akitoa majibu ya Serikali kuhusu changamoto zinazoikabili shule hiyo na jitihada za Serikali katika kukabiliana nazo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe.Ummy Mwalimu amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha uwekezaji unaenda sambamba na utunzaji wa mazingira ili kulinda afya za watu.

“Ndugu zangu sitafungia kiwanda, ila malalamiko haya tunayafanyia kazi kwa karibu ili kuhakikisha mazingira na afya za binadamu haziathiriki. Tunapenda wawekezaji lakini lazima wazingatie Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004” Ummy alisisitiza.

Akiwa katika mwendelezo wa ukaguzi wa Viwanda katika Jiji la Tanga, Waziri Ummy Mwalimu pia ametembelea Kiwanda cha kutengeneza Chokaa cha Neelkanth Chemical Limited na kumwagiza mwekezaji wa kiwanda hicho Bw. Rashid Hamoud (Liemba) kutumia teknolojia rafiki wa mazingira katika kiwanda hicho ili kupunguza changamoto za mazingira ambazo kwa hivi sasa zinalalamikiwa kutokana na kukithiri kwa vumbi, moshi na kelele zinazohatarisha afya za binadamu na viumbe hai wengine.