Home Mchanganyiko MBUNGE SANGU AIOMBA SERIKALI KUTATUA MGOGORO WA ARDHI JIMBONI KWAKE

MBUNGE SANGU AIOMBA SERIKALI KUTATUA MGOGORO WA ARDHI JIMBONI KWAKE

0

……………………………………………………………………………………..

MBUNGE wa Kwela(CCM),Mhe. Deus Sangu ameiomba  serikali kutatua mgogoro wa ardhi uliopo katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Pori la akiba la Uwanda iliyopo mkoani Rukwa kutokana na askari wanyamapori kuwanyang’anya wananchi mali zao.

Akiuliza maswali bungeni Mhe. Mbunge huyo amesema katika oparesheni za askari wanyamapori kumekuwa na tabia ya askari kunyang’anya wananchi mali ikiwamo mashine za boti na mali zingine za wananchi.

“Nataka kujua kauli ya serikali ni nini kwasababu askari hao wamekuwa wakikamata mali hizo na kuwa nazo zaidi ya miaka miwili au mitatu ambayo ni hasara pia kwa serikali na wananchi umasikini, niombe serikali kutokana na unyeti wa hali hii na je Wizara ipo tayari kuja kulionea uhalisia wa hali hii,”alihoji.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema kuwa masuala ya kisheria yanapokuwa chini ya mahakama wao wahifadhi hutegemea uamuzi wa mahakama.

“Lakini pia ushahidi tunabaki nao ikiwamo vitu alivyokamatwa navyo, Wizara ipo tayari kuangalia migogoro iliyopo kwenye eneo hilo na tutasuluhisha kadri inavyowezekana,”alisema.

Awali, amesema Pori la akiba Uwanda lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5,000 lilianzishwa mwaka 1959, na kutangazwa upya kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori namba 12 ya mwaka 1974, kwa Tangazo la Serikali Na. 275 la tarehe 8/11/1974.

Aiidha, amesema tangu mwaka 1974 hadi 2013 Pori hilo lilikuwa likisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na lilikabidhiwa rasmi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii tarehe 20/01/2014.

“Pori hilo linapakana na vijiji 11 vya Ilambo, Kilyamatundu, Mkusi, Kapenta, Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta na vijiji saba vya Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta ndivyo vyenye mgogoro na Pori la Akiba Uwanda,”amesema

Hata hivyo, alisema kutokana na mgogoro huo orodha ya vijiji husika iliwasilishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya migogoro iliyojumuisha Wizara nane na utekelezaji wa ripoti ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya Mawaziri hao chini ya uenyekiti wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndio italeta ufumbuzi wa mgogoro huo na mingine iliyopo.

“Tunaomba Mheshimiwa Deus pamoja na watanzania wote tuwe na subira wakati utekelezaji wa ufumbuzi unaratibiwa,”amesema Sangu