Home Biashara TRA MKOANI RUVUMA YAKUSANYA BIL.8.4 KATIKA KIPINDI CHA MIEZI 6

TRA MKOANI RUVUMA YAKUSANYA BIL.8.4 KATIKA KIPINDI CHA MIEZI 6

0

************************************************

Na Muhidin Amri,
Songea.

MAMLAKA ya mapato(TRA)mkoani Ruvuma, imefanikiwa  kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 8.442 sawa na asilimia  109 kati ya lengo walilopewa la  kukusanya shilingi bilioni 7.771   katika kipindi cha miezi sita kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo mkoani humo Amina Ndumbogani, wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu Mwaka wa fedha 2020/2021 kwa waandishi wa Habari ofisini kwake mjini Songea.

Aidha alisema, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Tra mkoani Ruvuma imepewa lengo la kukusanya shilingi bilioni  15.639, lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi wa mamlaka hiyo hadi kufika Desemba 2020 wamefanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya shilingi biliono 8.4 hivyo kuwa na matumaini ya kufika lengo la kukusanya shilingi bilioni 15.6.

Alisema, mbali na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi pia mafanikio hayo yametokana  na ushirikiano waliopa kutoka kwa  wadau wengine wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo Christina Mndeme na Wakuu wa wilaya tano za mkoa wa Ruvuma pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ambayo ni sehemu ya mafanikio hayo.

Alisema, anajivunia kuona  wadau mbalimbali  wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Chritina Mndeme,Wakuu wa wilaya za mkoa huo na  wafanyabiashara ndiyo waliofanikisha malengo ya Mamlaka  hiyo kuvuka malengo  katika kipindi cha nusu mwaka kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020.

Aidha alisema, kwa mwaka  huu wa fedha wameweka malengo mbalimbali kama mkakati wa kukusanya shilingi bilioni 15 walizopewa ambayo ni kupanua wigo kwa kuwatambua na kuwasajili wafanya biashara kwa  mfumo wa mtandao,kupita  mlango kwa mlango ili kuwabaini walipa kodi na wale wanaokwepa kulipa kodi na kuongeza nguvu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine za Efds.

Alisema, mbali na hilo mkakati mwingine ni  kuwafuatilia walipa kodi wenye madeni  ili kulipa  madeni yao kwa wakati kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

“kazi ya kukusanya kodi ni ngumu sana,lakini kutokana na jitihada kubwa zilizofanyika na wadau wengine kwa kweli ndiyo kwa kiasi kikubwa waliofanikisha malengo hayo”alisema Amina.

Alisema, mamlaka ya mapato inaendelea kuwakumbusha wafanya biashara na wananchi wote kwa jumla  kuwa msingi wa makadirio ya kodi kwa haki ni utunzaji sahihi wa kumbukumbu na ni wajibu na  kila mwenye sifa kulipa kodi stahiki za serikali.

Amina ameonya kuwa, mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutotumia vyema mashine za kielektroniki  katika biashara yake au kukaidi kutimiza wajibu huo wa kisheria atakuwa ametenda kosa na atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema, mfanyabiashara atakayekamatwa kwa kosa la  kutotumia mashine za Efds adhabu yake ni faini  kuanzia milioni 3 na isiyozidi milioni 4.5  au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa kodi ya mwaka 2015.

Pia, amewataka wanunuzi wote wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanadai risiti pindi wafanyapo manunuzi  kwani ni haki ya msingi na kisheria kwa kila mnunuzi, na kutofanya hivyo ni kosa linaloweza kupelekea kupata adhabu kali ikiwemo kutozwa faini kati ya shilingi 30,000 hadi  milioni 1.5

Alisema, Tra inategemea sana ushirikiano kutoka kwa wadau wote  katika suala zima la kukusanya mapato ya Serikali na kusisitiza,ni wajibu wa kila mwananchi kuonyesha uzalendo kwa kulipa kodi ili kuisaidia Serikali kutoa huduma bora na haraka zaidi.

Amina amesisitiza kuwa,  ni haki na lazima kwa mwananchi kudai risiti sahihi kila anunuapo bidhaa au huduma pamoja na kutoa taarifa ya upotevu wa mapato ili kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwahudumia Watanzania.