Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani akizungumza na watendaji pamoja na wafanyakazi wa shirika  la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 22,2021.

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani akisisitiza jambo kwa  watendaji pamoja na wafanyakazi wa shirika  la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 22,2021.

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma Frank Chambua akielezea walivyojipanga kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani, watendaji pamoja na wafanyakazi wa shirika  la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 22,2021.

  

Baadhi ya washiriki wa Kikao wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani alipokuwa akizungumza na watendaji pamoja na wafanyakazi wa shirika  la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 22,2021.

…………………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuboresha kitengo cha huduma kwa Mteja baada ya kubaini  kitengo hicho kutoa huduma zisizoridhisha kwa wateja.

Dk Kalemani ametoa agizo hilo leo  Januari 22,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na  watendaji pamoja na wafanyakazi wa shirika hilo mkoa wa Dodoma.

Dk.Kalemani amesema kuwa TANESCO mnatakiwa mjielekeze kibiashara kwa kuwatafuta wateja ili muweze kuboresha kitengo chenu.

“Nataka muwafuate wateja maana nasikia mnafuatwa na wateja mnakataa kuwasikiliza nendeni mkajionee Voda au Tigo jinsi wanavyowafuata wateja hivyo nataka muache tabia ya kuwakimbia wateja “amesema Dk.Kalemani
Aidha Dk.Kalemani amesema kuwa  ndani ya miezi sita ni lazima TANESCO mkoa wa Dodoma iongeze wateja maradufu huku akijiuliza kwa nini wateja hawajaunganishiwa umeme.
 Dk.Kalemani amewageukia Masavey na kuwaonya juu ya malalamiki ya wananchi kudanganywa katika kuwaunganishia wananchi umeme hali inayopelekea serikali kukosa wateja na mapato katika sekta ya umeme.

Waziri Kalemani amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuwekewa umeme kulingana na mahitaji yao na si mtazamo wa mtoa huduma hiyo.

“Wapo Watanzania wanaishi kwenye nyumba ambazo utadhani wanahama kesho lakini kumbe hahami, sasa wewe usiangalie nyumba yake ipoje, wewe mtundikie umeme,”amesisitiza Dk Kalemani

Hata hivyo Dk.Kalemani  amewataka watendaji kubadilika na kuondoa ukiritimba katika kuwaunganishia umeme wananchi huku akitoa angalizo hakuna kuwatoza wananchi Gharama za nguzo pamoja na  transformer

Aidha amesema ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikishiwa huduma ya nishati ya umeme februari 5,2021 wataanza utekeleza wa mradi wa kupeleka umeme katika vijiji 2159 vilivyobaki nchini.

Amesema mradi huo wa kufikisha umeme katika vijiji hivyo unatakiwa kutekelezwa kwa muda wa miezi 18.

Hata hivyo Dk Kalemani amewataka wafanyakazi wa shirika hilo kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kusababisha uwepo wa rushwa badala yake watoe huduma kwa wananchi kwa kufuata sheria.