*************************************************
Siku kadhaa kabla ya kufanyika Tamasha kubwa la Serengeti Music Festival wasanii wa kike wanaofanya vizuri katika muziki nchini Nandy na Palm D, wamewaita mashabiki wao kujazana Uwanja wa Uhuru siku ya Tarehe 26 Disemba, 2020.
“Nina surprise zao kibao siku hiyo, nataka mashabiki wetu waje kwa wingi lakini pia hata wasanii wenzangu wajiandae maana show ninayojipanga nayo siku ya Serengeti Festival sio ya kitoto,” alisema Nandy katika mahojiano kwenye kipindi cha Uhondo cha EFM.
Akizungumzia Tamasha hilo Msanii Palm D aliishukuru Serikali kwa ubunifu huo naye akawataka wasanii na mashabiki kujipanga vilivyo.
“Mimi nawaomba mashabiki waje tu pale Uwanja wa Uhuru, itakuwa show ya kufunga mwaka,” alisema.
Tamasha la Serengeti Festival linalounganisha sekta za sanaa na utalii limeandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau litafanyika jijini Dar es Salaam Disemba 26, 2020, na kiingilio kitakuwa Sh 5,000 tu.