Na Calvin Gwabara, Liwale.
ZAIDI ya shilingi milioni 957 zimepatikana kwenye vijiji kutokana
sekta ya misitu katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi na hivyo kuchangia katika
kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya na maji.
Hayo yamebainishwa na KatibuTawala wa Wilaya hiyo, Rajabu Kambangwa wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mchango wa sekta ya misitu na ushiriki wa wilaya hiyo kwenye uhifadhi
shirikishi wa misitu ya vijiji.
Alisema kuwa wilaya ya Liwale misitu ni chanzo kikubwa cha
mapato ya wilaya kwani katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 iliingizia serikali kiasi
cha shilingi bilioni 2.6 ikifuatiwa na sekta ya kilimo na hivyo kuifanya sekta ya
misitu kuwa sekta muhimu kwauchumi.
” Sisi kama wilaya tunanufaika sana na uwepo wa rasilimali hizi
kwa hiyo tunafarijika sana ujio wa miradi kama huu ya Uhifadhi shirikishi wa misitu
kwani inasaidia kuwajengea uwezo wananchi kwenye vijiji vyetu kuona umuhimu wa misitu
na uhifadhi wake kwa maendeleo endelevu lakini kubwa zaidi kuona misitusi ya serikali
bali ni mali yao” alisema Kambangwa.
Katibu Tawala huyo alisema kwenye Kijiji cha Likombola pekee
kiliingiza kiasi cha shilingi milioni 253 huku Kijiji cha Mtawatawa wakiingiza kiasi
cha shilingi milioni 122 ambazo zimetumika kufanya shunguli mbalimbali za
maendeleo kwenye vijiji hivyo ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa, Zahanati, Nyumba
ya Mtendaji wa Kijiji Pamoja naTrekta la Kijiji ambalo linawasaidia kwenye kilimo
kwa kukodishiana
kwa gharama za chini na kwa wakati.
Alisema pamoja na mafanikio hayo makubwa lakini swala la
uhifadhi bado linahitaji elimu kwa jamii maana Wananchi wasipoona faida za moja
kwa moja kwenye vijiji vyao hawawezi kuitunza wala kuilinda na hivyo kusababisha
misitu kupotea wakidhani ni mali ya Serikali.
Kwa upande wake Afisa Sera na Majadiliano wa Mtandao wa Jamii
wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)Elida Fundi alisema kuwa vijiji vinafanyakazi
kubwa na nzuri katika kuhifadhi misitu ya vijiji na hii inatokana na elimu na motisha
wanayoipata kwenye vijiji vyao baada ya kuvuna misitu hiyo kwa uendelevu.
Alisema MJUMITA kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo
na misitu wataendelea kushiriki kikamilifu kwenye kuzisaidia Halmashauri na vijiji
katika awamu hii ya tatu ya mradi kuweka mipango bora yamatumizi ya ardhi na utengaji
wa maeneo ya misitu ya hifadhi za vijiji ili itunzwe na kuvunwa kwa njia endelevu
ambazo zitatunza misitu hiyo.
Kwa upande wake Afisa Misitu wa wilaya hiyo, Nassoro Ali
Mzui alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo kwenye uhifadhi wa misitu hiyo
ni vitendea kazi hasa vyombo vya usafiri kama pikipiki na zana zingine kwani misitu
mingine inaukubwa wa zaidi ya hekta elfu 13 hivyo kuwawia vigumu kufanya doria na
kuizunguka kwa miguu.
Alisema kwa kuwa vijiji vinachangia asilimia kumi ya mapato yatokanayo
namisitu kwenda kwenye halmashauri wamekuwa wakifanya doria za pamoja na wanavijiji
na kamati zao za maliasili za kijiji pamoja na maafisa wa maliasili na askari
ili kusaidia kuongeza nguvu na kurahisha zoezi la ulinzi kwenye misitu hiyo.