Katibu wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara
Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, Seperatus Fella, akiweka mkakati wa namna
bora ya kukabiliana na biashara hiyo, alipokutana na wadau mbalimbali kwenye
mafunzo maalumu mkoani Singida juzi.
Afisa
wa Sekretarieti hiyo, Ahmad Said Mwen-dadi, akitoa mada kwenye mafunzo hayo.
wa
Sekretarieti hiyo, Alex Lupilya akitoa mada kwenye mafunzo hayo.
Picha
ya Pamoja ya baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo.
Na Godwin Myovela, Singida
WAKAZI mkoani hapa wametakiwa kuwa makini kabla ya
kuwaruhusu mabinti kuchukuliwa na kupelekwa maeneo mbalimbali nchini kwa kigezo
cha kutafutiwa au kufanya kazi za ndani, badala yake wahakikishe kwanza wanahusisha
uongozi wa Serikali ya Mtaa husika ili mchakato huo ufanyike kihalali.
Pia ‘dalali’ au mtu yeyote anayetaka kumchukua binti yako
hakikisha anakuwa na mdhamini wa kuwezesha kurahisisha mawasiliano ya mara kwa mara, lengo hasa ni
kuwa na uhakika wa mazingira ya usalama wa mwanao huko aendako.
Katibu wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara
Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Seperatus
Fella aliyasema hayo jana mkoani hapa, wakati akitoa mafunzo kwa wadau
mbalimbali ya namna ya kupambana na biashara ya usafirishaji binadamu.
“Singida ikitanguliwa na Wilaya ya Kondoa Dodoma ni miongoni
mwa mikoa ambayo wasichana wanachukuliwa na kwenda kutumikishwa kwa kufanyishwa
biashara za ngono kwenye majiji kama Dar es Salaam na kwingineko,” alisema
Fella.
Aliongeza kwamba tangu kuanza kwa mafunzo hayo kwa
kushirikiana na mashirika ya kitaifa na kimataifa mwaka 2017, mkoa wa Singida
ulikuwa bado haujafikiwa, na kinachofanyika kupitia mafunzo hayo ni kuwaelekeza
wadau mbinu bora za kuzuia na kukabiliana kisheria na biashara hiyo haramu.
Fella pamoja na mambo
mengine, alisema kwa muktadha wa kitaifa hali siyo ya kuridhisha sana kutokana
na mabinti wengi kuendelea kusafirishwa nje ya nchi kwa siri, kwa ahadi za
kutafutiwa ajira zenye mshahara mnono jambo ambalo sio kweli, na kinyume chake
hugeuzwa watumwa kwa kufanyishwa biashara za ngono na madawa ya kulevya kwa
maslahi ya waliowasafirisha.
“Tunaendelea na juhudi za kuwaokoa, na hivi karibuni
tumewaokoa mabinti wa kitanzania waliokuwa wakitumikishwa kama watumwa kutoka
Iraq, Malaysia na India…na wametueleza kuwa bado wamewaacha wenzao wengi
wakiendelea kuteseka,” alisema Fella.
Kwa upande wake Afisa wa Sekretarieti hiyo, Ahmad Mwen-Dadi,
alisema biashara hiyo ni ya tatu kwa kuingiza fedha nyingi ikitanguliwa na ile
ya Madawa ya Kulevya na Uuzaji wa Silaha Haramu, hivyo ni jukumu la kila raia
wa Taifa la Tanzania kuchukua tahadhari kwa ulinzi madhubuti wa watoto na
mabinti kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Alisema madalali wa biashara hiyo wanapokutana na mabinti
wamekuwa wakiwahadaa kwenda kufanya kazi kwenye mahoteli makubwa, maduka
makubwa (supermarkets), Saluni na kazi nyinginezo zenye maslahi makubwa, jambo
ambalo hatimaye huwashawishi mabinti walio wengi kutoroka bila kuaga wazazi.
“Wengi wanasafirishwa kupelekwa nchi za Thailand, China,
Malaysia, Bangladesh na hata Iraq na wakifika huko wanajikuta kazi
walizohaidiwa sio wanazifanya. Wengi tuliowaokoa wanasema wenzao wapo katika
hali mbaya ya kutumikishwa kikatili mpaka pale watakapomaliza kulipa deni la
gharama za kuwasafirisha hadi kufika kwenye hizo nchi,” alisema Mwen-Dadi.
Aidha, alitoa tahadhari kwa wana-singida na taifa kwa ujumla
kuwa makini kutokana na ukweli kwamba kwa sasa usafirishaji wa ndani kutoka
mkoa mmoja kwenda mwingine hadi Zanzibar umeuzidi ule usafirishaji wa watoto na
mabinti wa kitanzania kupelekwa nje.
“Naomba sana tuwe makini, bado hatujafikia umasikini wa
kuacha watoto na mabinti zetu kwenda kudhalilishwa na kufanyiwa vitendo vya
ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu. Mapambano dhidi ya biashara hii haramu
ni jukumu letu sote kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa,” alisema.
Wadau waliopata fursa ya kushiriki mafunzo hayo ni Maafisa
Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Singida, Mashirika yasiyo ya
kiserikali, kikiwemo Kituo cha Faraja na Jeshi la Wokovu, Jeshi la Polisi,
Uhamiaji na Maafisa Serikali za Mitaa.
Mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yanalenga kuelimisha na
kutoa taswira ya namna bora ya kukabiliana kisheria na biashara haramu ya
usafirishaji binadamu, kuendesha kesi, kupepeleza na kutoa misaada ya utambuzi
na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.