Home Uncategorized RC KIGOMA APONGEZA TRA KUJA NA KAMPENI YA ELIMU KWA MLIPAKODI

RC KIGOMA APONGEZA TRA KUJA NA KAMPENI YA ELIMU KWA MLIPAKODI

0

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akiongea na kutoa baraka zake kwa timu ya Maafisa wa Kampeni ya Utoaji Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla ya kuanza kwa kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi (Mlango kwa Mlango) inayoanza leo 17 hadi 30 Agosti, 2020 mkoani Kigoma.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma, Bw. Jackob Mtemang’ombe akitoa utambulisho mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye kuhusu ugeni wa timu ya Maafisa wa Kampeni ya Utoaji Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA ambao wapo kwa ajili ya Kampeni ya kutoa elimu kwa Mlipakodi (mlango kwa mlango) mkoani hapo. Maafisa wa Kampeni ya Utoaji Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiwa ndani ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wakati walipomtembelea kwa ajili ya kujitambulisha kabla ya kuanza kwa zoezi la utoaji elimu kwa Mlipakodi (mlango kwa mlango) mkoani hapo. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye (kulia) akiagana na Kiongozi wa msafara wa timu ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Julius Mjenga wakati walipomtembelea ofisini kwake ajili ya utambulisho kabla ya kuanza Kampeni ya kutoa elimu kwa Mlipakodi (mlango kwa mlango) mkoani hapo.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Kampeni ya Utoaji Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati walipomtembelea ofisini kwake ajili ya utambulisho kabla ya kuanza Kampeni ya kutoa elimu kwa Mlipakodi (mlango kwa mlango) mkoani hapo.

PICHA ZOTE NA TRA.

***********************************

MWANDISHI WETU-KIGOMA

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema amefurahishwa na kampeni ya elimu ya kodi ya mlango kwa mlango inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kigoma na kwamba wafanyabiashara wanaohofia kunyang’anywa faida zao na wanatakiwa kutumia nafasi hiyo kuhoji maswali na kupata elimu.

Akizungumza baada ya kutembelewa na maafisa wa TRA kutoka makao makuu waliofika mkoani hapa kwaajili ya kuendesha kampeni ya elimu ya kodi mlango kwa mlango, Andengenye amesema huu ni wakati wa wafanyabiashara wa kukidhi kiu yao ya maswali kuhusu kodi pamoja na changamoto wanazokutana nazo ili waweze kutatuliwa na maofisa hawa wa TRA ambao wamekuja kukusanya pesa ya serikali inayotokana na biashara wanazofanya.

Amesema kampeni hiyo itawawezesha kujua kuwa pesa zinazokusanywa sio za TRA na kwamba ni za serikali ambazo zitamgusa kila mmoja kutokana na miradi ambayo inatekelezwa na serikali.

“Nawashauri wafanyabiashara watoe ushirikiano kwa maofisa wetu na sehemu ambayo watakuwa hawajaelewa wanatakiwa kuuliza ili kuelekezwa na kwamba huu ni wakati wao na kwamba lengo ni kujenga urafiki baina ya TRA na walipakodi,” anasema Andengenye.

Naye meneja wa TRA mkoa wa Kigoma, Jackob Mtemang’ombe  anasema kuwa mkakati wa TRAni kuhakikisha inaeneza elimu ya kodi kwa kila mwananchi kwa urahisi na kwamba kampeni hii ya mlango kwa mlango ni nzuri kutokana na kuwa elimu itawafikia kwa urahisi kutokana na kuwa watafikiwa katika maeneo yao.

Anasema ni vingumu kwa walipakodi kuacha biashara zao na kuhudhuria semina za kodi hivyo TRA imeamua kuwafata ili kuwarahisishia ikiwa ni pamoja na kuona mazingira wanayofanyia biashara zao na changamoto wanazokutana nazo.

“Ni rahisi kumuelimisha mlipakodi akiwa katika eneo lake la biashara ukilinganisha akiwa mbali na kwamba baada ya kuwaelimisha ndipo tutaanza kufuata sheria kutokana na kuwa watakuwa wameshapata uelewa,” anasema Mtemang’ombe.