Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Kabwe wilayani Nkansi baada ya kuzindua bandari ya Kabwe , Julai 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua bandari ya Kabwe wilayani Nkansi, Julai 5, 2020. Wa pili kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, kushoto ni Mbunge wa Nkansi, Ally Kesi, Wa nne kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo na wa pili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Baraka Mdima. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano , Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kushoto) wakati alipowasili kwenye eneo la Kabwe wilayani Nkansi kuzindua bandari, Julai 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia baada ya kuzindua bandari ya Kabwe wilayani Nkansi, Julai 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipowasili kwenye eneo la Kabwe wilayani Nkansi kuzindua bandari Julai 5, 2020. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua bandari ya Kabwe wilayani Nkansi, Julai 5, 2020. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Josephat Kandege na wapili kulia ni Mbunge wa Nkansi, Ally Kesi.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
**********************************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua Bandari ya Kabwe uliyojengwa na kampuni ya Kitanzania ya Sumry’s Enterprises kwa thamani ya sh. bilioni saba.
Ujenzi huo wa Bandari ya Kabwe yenye eneo la ukubwa wa mita za mraba 10,864 unalenga kuongeza tija katika shughuli za bandari kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika na kupanua fursa za kibiashara.
Waziri Mkuu amezindua bandari hiyo leo (Jumapili, Julai 05, 2020) wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa. Bandari hiyo imenjengwa Kata ya Kabwe, wilayani Nkasi, Rukwa.
Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya Sumry’s Enterprises kwa kujenga vizuri mradi huo . “Rais wetu Dkt. Magufuli amesema Watanzania tunaweza na huyo mkandarasi amedhirisha hilo.”
“Hizi ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuhakikisha maendeleleo yanawafikia wananchi wote bila ya ubaguzi.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi washirikiane na Serikali katika kulinda miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu.
“Hatuna historia mbaya hapa, endeleeni kudumisha uaminifu na uadilifu ili bandari hii iwe ni mahali salama kwa abiria na mizigo. Bandari hii itaongeza fursa kibiashara kati yetu na nchi jirani.”
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Dkt. Baraka Mdima amesema mradi huo utakuwa chachu ya kukuza uchumi na kuboresha usafiri.
“Mradi huu wa bandari utaboresha usafiri wa majini kwa wananchi waishio kandokando ya Ziwa Tanganyika hususani wilaya ya Nkasi na katika kata ya Kabwe na vijiji vinavyoizunguka.”
Amesema mradi umehusisha ujenzi wa gati la kupaki meli lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za kubeba abiria na mizigo zenye urefu hadi mita 75 na miundombinu mingine ya bandari kama jengo la kupumzikia abiria, majengo ya ofisi, nyumba za kuishi watumishi na eneo la mgahawa.