**********************************
Na Farida Said
Makatibu wakuu na Manaibu makatibu wameridhidhwa na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa JULIUS NYERERE MW2115 kutokana na kazi inayofanywa na Mkandarasi wa mradi huo ambao wanasimamiwa na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO).
Walisema hayo walipotembelea mradi huo jana kujionea mitambo ya kusaga mawe na kutengeneza zege, handaki la kuchepusha maji na sehemu ya kuvunia maji (power intake) katika mradi huo.
Katika hatua nyingine wamelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi kubwa inayoifanya katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, ambapo kukamilika kwake kutawasaidia Watanzania kukuza uchumi wao kwa kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo ambayo vinahitaji nishati ya umeme.
Wakiongea katika ziara hiyo wakiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Aloyce Nzuki, wamesema kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia katika wizara zao kuimarisha mambo mbalimbali hivyo wameiomba Tanesco kuendelea kumsimamia vizuri mkandarasi kama wafanyavyo sasa.
Awali akitoa taarifa kwa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu waliotembelea Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere MW2115, Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Mushubila Kamuhabwa amesema mpaka sasa mradi umefikia asilimia 86 ya mpango kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika wa Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Dk Tito Mwinuka amewahakikishia makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu pamoja na Watanzania kwa ujumla kuwa mradi unaendelea vizuri na utakamilika kwa wakati.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi alisema serikali itaendelea kutekeleza mradi huo kama walivyokubalina na mkandarasi na kwamba hadi sasa wametoa Zaidi ya Sh trilioni moja kwa ajili ya mradi huo ambao utagharimu Sh trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake Juni 2022.