WAMJW- Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua kituo cha huduma za simu kwa wateja ambacho kazi kubwa ni kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya ikiwamo magonjwa milipuko.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Ummy Mwalimu amesema kituo hicho kina uwezo wa kupokea simu 1000 kwa wakati mmoja na kuunganisha vituo vitano kwa wakati mmoja.
Amesema kazi ya kituo hicho ni kupokea maoni, taarifa, maswali na ushauri kuhusu masuala mabalimbali yanayohusu sekta ya afya na amewataka wananchi kupiga simu 199 ili wapate huduma na walioko nje ya nchi wanapaswa kupiga namba 0800110124.
Amewataka wananchi watakaopiga simu kuwa wastaarabu, kutumia lugha ya staha na kutoa taarifa sahihi ambazo zitasaidia Serikali na Wizara ya Afya kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
Amefafanua kwamba kituo hicho kitatumika kutoa elimu na miongozo mbalimbali kuhusu masuala ya afya na kitakuwa na watalaamu 150 wakiwamo wataalamu wa afya, wauguzi na madaktari.
Amesema endapo Wizara ya Afya itaweza kutumia vizuri Tehama, itachangia changamoto mbalimbali zilizoko kwenye sekta ya afya, huku akiitaka jamii itambue kinga ni bora kuliko tiba na kwamba Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka minne na nusu imefanya vizuri katika masuala ya tiba na kinga.
“Hapa nimeelezwa kwamba kituo hiki kitahudumia kwa saa 24 kwa mwaka na kina uwezo wa kuhudumia watu 300,000 kwa siku,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya, amependekeza kituo hicho kipatiwe jina la ‘Afya Call Centre’ badala ya kituo cha huduma za simu ambacho kitakuwa kikishughulikia magonjwa yote.
“Kituo hiki kitakuwa kikizungumzia chanjo kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja, tutazungumzia masuala ya liche kwa kina mama wenye umri wa kuzaa, lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, masuala ya huduma ya uzazi ya mama na mtoto, tutanzungumzia mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu na masuala ya tiba,” amesema.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema kituo hicho kitatumika kutoa taarifa sahihi kwa jamii na kwa wakati.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt. Ama Kasangala alimweleza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwamba kazi kubwa ya kituo hicho ni kupokea maswali, maoni na ushauri kutoka kwa wananchi na kufanyiwa kazi na wataalamu wa afya.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani Tanzania (WHO), Dkt. Tigest Ketsela amepongeza kuanzishwa kwa kituo hicho kwa kuwa kitatumika kujibu maswali ya wananchi kuhusu magonjwa mbalimbali.
Dkt. Ketsela taarifa zitakazotolewa katika kituo hicho zitatumika kuandaa jumbe za kuielimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
Wadau wengine walioshiriki katika ujenzi wa kituo hicho wameipongeza Serikali na Wizara ya Afya kwa kizindua kituo hicho kwani kitasaidia kujenga imani kubwa kwa wananchi katika masuala yanayohusu afya.