********************************
NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania(JOWUTA) kimesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari nchini kuendelea kuzingatia maadili, kanuni na sheria katika utekelezaji wa majukumu yao katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu COVID19.
Akitoa salamu za maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Habari Duniani leo, Mwenyekiti wa JOWUTA, Claud Gwandu alisema uhuru wa habari, maadili, haki, usawa ni nguzo muhimu za kuzingatiwa na wanahabari nchini katika kipindi hiki kigumu ambapo dunia nzima inapambana na COVID-19.
“Tunapotekeleza majukumu yetu muhimu ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, tunapaswa kuchukua tahadhari zote za kiusalama kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa vifaa kinga kama barakoa na kufuata maelekezo ya wataalam wa afya ili kuepuka kupata maambukizi ya virusi vya corona.
Alisema JOWUTA inaunga mkono kauli mbiu ya Siku ya Uhuru wa Habari 2020 ambayo inasitiza waandishi kufanya kazi bila hofu ua upendeleo ili kuonesha umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari hasa kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.
Gwandu aliwataka waandishi kuadhimisha siku hii kwa kukumbushana kusimamia maadili ya uandishi wa habari kwa kuwa wao ni kioo cha jamii.
“Tunaadhimisha siku ya uhuru wetu huku duniani ikipitia wakati mgumu wa mapambano dhidi ya COVID-19 ni imani yangu kuwa tutasimamia maadili, uadilifu, haki, usawa, kanuni na sheria zinazosimamia taaluma yetu,” alisema.
Mwenyekiyi huyo alisema iwapo kundi hili litakuwa na mshikamano na ushirikiano na wadau wa maendeleo na serikali malengo ya kuifikisha Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati itafanikiwa.
“Nasisitiza umuhimu wetu kwenye jamii asitokee kati yetu anakubali kutumika kwa maslahi ya mtu binafsi.Tambua utakuwa umesaliti Watanzania zaidi ya milioni 50,” alisema.
Gwandu alitumia siku hiyo kuwahamasisha waandishi wa habari nchini kujiunga na JOWUTA ili kwa pamoja waweze kupigania haki zao za msingi.
Alisema jukwaa pekee ambalo waandishi nchini wanaweza kufikisha malalamiko na changamoto zao ni JOWUTA hivyo hawanabudi kujiunga kwa sasa.