serikali inahakikisha wananchi wanapata umeme kwa gharama nafuu
NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
Tanzania imetajwa kuwa ni nchi ya kwanza barani Africa kuwawezesha wananchi waishio vijijini kupata umeme kwa gharama nafuu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawezesha wananchi kukabiliana na changamoto ya kiuchumi kwa kukuza miundombinu wezeshi ya uchumi vijijini.
Akizungumza wakati wa ziara ya awamu ya pili ya Iringa Mpya Mkuu wa mkoa wa Iringa Ali Hapi alisema kuwa serikali imekuwa ikitekeleza ahadi ya kutoa huduma ya nishati ya umeme vijijini kwa gharama ambazo hakuna nchi nyingine barani Afrika inatoa.
Akiwa katika tarafa ya Kiponzelo Hapi alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuwa na subira wakati serikali imejipanga kuhakikisha inamalizia kuwapa umeme katika vitongoji vyote nchi nzima vilivyobaki.
“Rais wetu amekuwa anapambana kila kukicha kuhakikisha wananchi wanakuza uchumi wao na kupata maendeleo kwa wakati na ndio maana nishati ya umeme imekuwa ikitolewa kwa gharama nafuu nchi nzima” alisema Hapi
Aidha Hapi aliongeza kuwa viongozi wote waliopo ngazi za chini wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa nafasi zao kiufasaha na kuhakikisha wanatatua changamoto za wananchi ili kuhakikisha wanakuza uchumi wa wananchi wa kawaida kuanzia ngazi za vitongoji.
Pia aliwataka wananchi wote kuacha tabia ya kuendekeza maneno ya kinafiki kwa watendaji wa serikali kwa kuwazushia taarifa ambazo zitawavunja moyo kufanya kazi kwa nguvu ili kumsaidia Mh. Rais kuijenga Tanzania mpya ya viwanda na biashara nchini.
Alisema “ tumetumwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasikiliza na kuwatataulia changamoto zilizopo ndani ya uwezo wetu, nyinyi ndio ambao mmetuajiri kwahiyo ni lazima tuwatumikie na kuhakikisha mnakuwa na maisha mazuri na kupunguza umasikini katika kaya zenu”
Akijibia baadhi ya hoja za wananchi kaimu meneja wa tanesco mkoa wa Iringa injia Festo Ndamenya alisema kuwa serikali imekuwa ikigharamia gharama kubwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme kwa kulipia kiasi cha shilingi 27000 tu kwa kila nyumba ambayo inahitaji nishati hiyo kwa matumizi ya kimaendeleo.
Ndamenya alisema kuwa umeme wa REA umekuwa na awamu tatu tofauti ambazo kwa kifupi zimeleta maendeleo makubwa ya kiuchumi kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya Iringa Richard Kasesera alisema kuwa wananchi wanatakiwa kutambua umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii katika kukuza pato lao ndani ya kaya ikiwa ni pamoja na kujali afya zao kwa kujiunga na bima ya afya ili waweze kutibiwa kwa ufasaha.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa tarafa Kiponzelo walitoa changamoto zao, ikiwa ni pamoja na ubovu wa barabara, wawekezaji kutojali maslahi ya vijiji, uhaba wa madawa kwenye vituo vya afya, na changamoto ya ardhi kupewa wawekezaji bila ridhaa ya mikutano ya vijiji