Serikali ya Tanzania na China zimetoa tamko la pamoja kuhusu hali za watanzania walioko nchini China na hatua zinazochukuliwa na nchi hiyo kukabiliana na virusi vya Corona.
Tamko hilo la pamoja limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) pamoja na Balozi wa China hapa Nchini Mhe Wu Ke wakiwa wameambatana na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu Jijini Dar Es Salaam.
Akitoa tamko hilo Waziri Kabudi amesema Ubalozi wa China umeomba fursa ya kukutana na Serikali ya Tanzania kwa nia ya kueleza kwa pamoja hali ilivyo nchini China,hatua zinazochukuliwa na Serikali ya China kukabiliana na maradhi hayo ili kuzuia kusambaa katika maeneo mengine duniani sanjari na hali ilivyo kwa Watanzania wanaoishi Nchini humo.
Kwa upande wake Balozi wa China hapa Nchini Mhe Wu Ke amewaondoa wasiwasi Watanzania wote wakiwemo Wazazi na Ndugu wa wanafunzi zaidi ya 4000 hususani wanafunzi 400 walioko Hubei katika Mji wa Wuhan ambapo panatajwa kama kitovu cha Virusi vya Corona kwa kusema wako salama na hakuna hata mmoja aliyeathiriwa.
Ameongeza kuwa Serikali ya China kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani linachukua hatua zote kuhakikisha kuwa virusi hivyo havisambai katika maeneo mengine hasa baada ya shirika hilo kuutangaza ugonjwa huo kama janga,ikiwemo jitihada za China kujenga Hospitali maalum kwa ajili ya kuwatibu wale wote watakaoathirika.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema mpaka sasa hakuna mtu yeyote awe rai wa Tanzania ama wakigeni aliyethibitika kuwa na virusi hivyo na Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki na za dharura ikiwemo kuwapima watu wote wanaowasili Nchini kupitia viwanja vya ndege na aina nyingine za usafiri.
Ameongeza kuwa tayari serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imeimarisha uwezo wa kuwapima ndani ya Nchi mtu yeyote atakayeshukiwa wa virusi hivyo badala ya kupeleka sampuli hizo sehemu nyingine ikiwa ni pamoja na nje ya nchi.
Amesisitiza kuwa Mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote ama mtu yeyote aliyeshukiwa ama kuthibitishwa kuwa na Virusi vya Corona na tayari Wizara imetenga maeneo manne kwa kuangalia maeneo yaliyoko katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam,Mwanza na Kilimanjaro pia mazungumzo yanaendelea ili Zanzibar nayo iweze kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wagonjwa ama washukiwa wa homa ya Corona.
KATIKA HATUA NYINGINE, Tanzania imesema hakuna katazo kwa Mtanzania yeyote aliyeko nje ya Nchi, China ikiwemo anayezuiwa kurudi Tanzania pindi atakapo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Mnyepe amewaondoa wasiwasi Watanzania hasa wale wanaotaka kusafiri kwenda ama kurudi kutoka China,na kwamba wale wanaotaka kusafiri kwenda China tayari waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa ameshatoa maelekezo lakini kwa wale wanaotaka kurudi kutoka China Ubalozi wa Tanzania Nchini China unashirikiana nao kuwarejesha Tanzania kwa wale wanaotaka na kwamba hakuna katazo la kurejea Tanzania.