…………………………………………………………………………………….
Na Magreth Kinabo- Mahakama
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amesema Bunge litashirikiana na Serikali kuhakikisha Mahakama ya Tanzania inapate rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati.
Akizungumza leo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria iliyoambatana na matembezi maalum ya kilomita tano yaliyoanza kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu Dodoma hadi kwenye maonesho, ambayo yanaendelea katika Viwanya vya Nyerere Square, aliipongeza Mahakama kwa maonesho mazuri.
‘’Bunge litashirikiana na Serikali, kuhakikisha Mahakama inapata rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati,’’ alisema Spika.
Aidha Spika huyo alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma, wafike katika viwanja hivyo ili wajue haki zao na kupata elimu ya sheria kwa kuwa Mahakama si sehemu ya kuogopwa.‘ wananchi wakielewa haki zao hawatadanganywa,’ alisisitiza.
Spika huyo, aliipongeza Mahakama kwa kauli mbiu yake ya mwaka huu inayosema ‘Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.’ Kwa kuwa inasaidia kufikisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi imara na viwanda.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge alitoa shukrani kwa Mahakama kujenga majengo ya Mahakama Jumuishi na Ofisi za Makao Makuu jijini Dodoma.
Katika maonesho hayo, Spika pia alizindua Vitabu Vitatu vya Muongozo wa Kusikiliza Mashauri Mahakamani vinatumika Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mkoa na Mahakama Kuu ( A hand book for Magistartes in Primary Courts, A guick reference for Magistrates in the District Court and Courts of Resident Magistrtes in Tanzania and Bench Book for Judges in Tanzania).
Akizungumzia kuhusu vitabu hivyo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, alisema vitabu vimeshawekwa kwenye Tovuti ya Mahakama ya Tanzania.
Wiki ya hiyo imeanza Januari 31, mwaka huu na inatarajia kumalizika Februari 5, mwaka huu, ambapo kilele chake cha Siku ya Sheria nchini kitafanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu J. K. Nyerere.
Mgeni rasmi katika kilele hicho, anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.