Home Mchanganyiko RMO MIRERANI AVALIA NJUGA ELIMU KWA KUPAMBANIA MADARASA 10 YA WANAFUNZI 400 

RMO MIRERANI AVALIA NJUGA ELIMU KWA KUPAMBANIA MADARASA 10 YA WANAFUNZI 400 

0

Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima akizungumza juu ya uchangiaji wa shilingi milioni 200 milioni za ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari Mirerani Benjamin Mkapa na Tanzanite, kushoto ni Mwenyekiti wa kamati ya elimu, afya na maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kilemp Ole Kinoka na Ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Evence Mbogo.
**************************************
OFISA madini mkazi wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Daudi Ntalima amevalia njuga changamoto ya upungufu wa madarasa ya shule za sekondari baada ya kuingilia kati ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa ili wanafunzi 400 wapate elimu. 
Wanafunzi waliofaulu 700 wa shule za sekondari Mirerani Benjamin Mkapa na Tanzanite, miongoni mwao 400 wanakabiliwa na ukosefu wa madarasa hivyo kuhofia kutembelea umbali wa kilomita 10 kwenda shule ya sekondari Naisinyai 
Ntalima akizungumza jana alisema ameweka mikakati ya kuhakikisha wadau wa madini wanachangisha sh200 milioni ili madarasa 10 yajengwe kwenye shule hizo mbili na wanafunzi hao waaanze kusoma mapema mwakani. 
Alisema baada ya kusikia changamoto ya ukosefu wa madarasa 10 kwa wanafunzi 400 waliotarajiwa kuanza kidato cha kwanza mwakani aliona upo umuhimu wa kutatua tatizo hilo kupitia wadau wa madini. 
“Kuna sheria inayowabana wadau madini kurudisha kile kidogo walichopata kupitia shughuli za kijamii CSR hivyo tumepanga tujenge madarasa hayo kupitia wamiliki wa migodi, wachimbaji, wanunuzi na madalali,” alisema Ntalima. 
Alisema atahakikisha mpango huo unakuwa endelevu ikiwemo kufungua akaunti benki ili wadau hao wachangie maendeleo na kuondokana na dhana iliyopo kuwa wadau wa madini ya Tanzanite hawachangii maendeleo. 
Ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Evence Mbogo alisema fedha hizo za wadau zitasimamiwa ipasavyo ili kutimiza lengo kwani zitakuwa kwenye mikono salama. 
Mbogo aliahidi ndani ya wiki mbili kufungua akaunti kwenye benki ambayo itakuwa maalum kwa wadau wa madini kuchangia maendeleo ya eneo hilo. 
Mmoja kati ya wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite, Fatuma Kikuyu alipongeza ubunifu uliofanywa na Ntalima hadi kusababisha ujenzi wa madarasa hayo ya shule yatakayowasaidia wanafunzi hao. 
Alisema tangu ajishughulishe na madini ya Tanzanite akiwa msichana hajaona ofisa wa madini mwenye moyo wa kuijali Mirerani kama Ntalima. 
Meneja wa mgodi wa Saniniu Laizer, Kirya Laizer alisema juhudi hizo za RMO kuwabana wadau wa madini wachangie elimu kinapaswa kupongezwa na wapenda maendeleo. 
“Madini ni rasilimali ambayo inaweza kuisha lakini madarasa hayo yatatumika hata miaka 100 na wanafunzi hivyo wadau wa madini wanapaswa kutekeleza uchangiaji huo kwa ajili ya maendeleo ya jamii.