Home Mchanganyiko BAADHI YA WAKAZI MTAMBANI WAMLILIA LUKUVI,NDIKILO NA KAWAWA KUPEWA HAKI YAO

BAADHI YA WAKAZI MTAMBANI WAMLILIA LUKUVI,NDIKILO NA KAWAWA KUPEWA HAKI YAO

0

****************************************

NA MWAMVUA MWINYI, Bagamoyo
Nov 27
Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Mtambani Kimarang’ombe Kata ya Nianjema Bagamoyo mkoani Pwani, wanaodai kutapeliwa ardhi yao ya hekari 34 ,wamemtaka Waziri wa ardhi William Lukuvi ,serikali ya mkoa na wilaya kuwasaidia kurejeshewa eneo lililovamiwa ili waishi kwa amani.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao na Waandishi wa habari katika eneo hilo Fatuma Ramadhani, Hussein Temo, Isdory Mwepong’we na Makolega Turuka, walielezea masikitiko yao ya kutakiwa kuondoka katika eneo waliloishi miaka 40 sasa.
Fatuma alisema ,walifika kwenye eneo hilo mwaka 1974 wakianza kulima, kabla ya Mkuu wa wilaya miaka hiyo Shaaban Kandoro kufika katika eneo hilo, akimtaka mmiliki na kukuta pori kubwa.
“Alipofika alituuliza mmiliki, na alitoa miezi mitatu kwa viongozi wamtafute mmiliki, kama hajajitokeza eneo hilo ataligawa kwa wananchi waliokuwepo, huku akiwataka viongozi wa kijiji wakati huo na kata kumfatuta,” alisema Fatuma.
Nae Hussein Temo alieleza baada ya muda aliouweka Mkuu huyo wa wilaya wakati huo kumalizika pasipo kupatikana mmiliki, akaamua kuwagawia eka mojamoja kila mtu akaanza kuyaendeleza kwa kilimo, huku wengine wakijenga nyumba za muda.
“Tulishangazwa ulipofika mwaka 2010 kuwaona watu wakiwa na darubini wanapima maeneo hayo pasipokujulishwa, tuliitana na kukubaliana kwenda kwa viongozi wa Kijiji, ambapo Mwenyekiti akatuambia hata yeye hana taarifa ya zoezi hilo,” alisema Temo.
Kwa upande wake Makolega Turuka alihoji uhalali wa Omary Sud ambaye kwa sasa ni marehemu, ambaye ni mkazi wa Bagamoyo alikuwa wapi kwa zaidi ya miaka 40, na kusema kuna mchezo mchafu wa kutaka kuwaondoa wananchi hao kisha wapige bei.
“Kesi ilifunguliwa mahakamani na kufikia 2010 Sud alikiri eneo hilo si lake ,na kesi ilifutwa kisha kusema walionunua kupitia yeye warudishe fedha ama kuwalipa fidia wazee hao”
Akizungumzia sakata hilo,ofisa ardhi wilayani hapa Wendeline Izana alisema kuwa, taarifa hizo alipatiwa na Ofisa Mtendaji Kata kwamba eneo hilo ni la Omari Sud.
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Yussuph Mgala alisema kwamba analitambua eneo hilo miaka mingi kabla hajashika wadhifa huo, na kwamba linamilikiwa na Sud kabla ya kuwapatia wananchi hao walime mazao ya muda mfupi, na kwamba 2010 alifika kwa ajili ya kupima viwanja.
Mtendaji Kata wa Nianjema Sezary Madasha alifafanua, anatambua eneo hilo ni la Sud, hivyo aliwashauri wananchi hao wakafungue mashitaka katika mahakama ambayo ndio yenye maamuzi kisheria.