**********************************
WADAU wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameunga mkono uamuzi wa Serikali wa madini ghafi ya Tanzanite kutotolewa nje ya ukuta unaozunguka migodi hiyo bila kuongezwa thamani ifikapo Novemba mosi mwaka huu.
Wadau wa madini ya Tanzanite wakiwemo, wamiliki wa migodi, wachimbaji, wanunuzi, madalali, wachakataji, wafanyabiashara na maofisa wa Tume ya madini, walikutana jana kwenye ofisi za madini Mirerani.
Mmoja kati ya wachimbaji madini hao, Samuel Rugemalira alisema suala la kuhifadhi madini ndani ya ukuta ili yaongezwe thamani ni zuri kwani kutakuwa na usalama zaidi tofauti na kuyaweka nyumbani.
Rugemalira alisema yeye ameelewa vizuri maelezo ya serikali yaliyotolewa kuhusu katazo la kutoa ndani ya ukuta unaozunguka migodi, madini ghafi bila kuongezwa thamani.
Ofisa habari wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini nchini Femata Dk Bernard Joseph alisema serikali inapoamua kufanya jambo lake lazima itakuwa imejipanga kikamilifu katika utekelezaji wake.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo alisema miundombinu ya kufanikisha zoezi hilo inapaswa kuandaliwa kwani uzalishaji ukifanyika kwenye migodi mingi kutakuwa na changamoto.
Mchimbaji mwingine Elisafi Lema alisema siyo jambo baya kutunza madini ndani ya ukuta ila siyo madini yote yanayofaa kuongezwa thamani.
Ofisa madini mkazi wa mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima alisema uamuzi huo una manufaa makubwa kwa wadau wa madini na serikali kwa ujumla.
Ntalima alisema wachimbaji wa madini ya Tanzanite watafaidika zaidi wakifanya biashara pindi wakiuza madini yasiyo ghafi ambayo yameongezwa thamani.
Aliwataka wadau wa madini kuanza mchakato wa kujenga ofisi kwani wameshatenga maeneo ya ndani ya ukuta huo kwa ajili ya zoezi hilo.