*************************************
Ripoti ya Utafiti wa Taasisi ya usimamizi na uwekezaji wa kifedha Afrika ABSA imetoa orodha mpya ya mwezi Oktoba, 2019 ya masoko ya uwekezaji na kuonesha Tanzania ipo nafasi ya saba ikilinganishwa na mwaka 2018 ilipokuwa kwenye nafasi ya 15 kati ya nchi 20 za Afrika zenye mazingira mazuri ya uwekezaji.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe Jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na maendeleo ya uwekezaji Nchini.
“Uzoefu wa ‘Absa Group’ katika mambo ya Fedha na Uwekezaji na matokeo ya utafiti wake, yanatudhihirishia kuwa juhudi zinazofanya na serikali za kuboresha mazingira ya uwekezaji zinaifanya Tanzania kuwa kivutio bora cha uwekezaji kwenye bara la Afrika” alisema Mwambe.
Mwambe amebainisha kuwa tafiti kubwa za kimataifa zinaonyesha mazingira na hali ya uwekezaji nchini itaendelea kuimarika huku akitolea mfano uchumi wa Tanzania kuendelea kukua kwa kasi kubwa ya asilimia 7.0 kwa miaka minne mfululizo, ambapo kwa sasa nchi inashika nafasi ya tano kati ya Mataifa 10 Duniani yenye uchumi unaokua kwa kasi kutokana na hatua za makusudi zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kukuza sekta binafsi ambayo ni injini ya ukuaji wa uchumi.
Aidha ameendelea kuwashauri Wawekezaji Duniani kuja kuwekeza nchini Tanzania kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji na usalama na kufafanua kuwa Serikali inaendelea na maboresha ya miundombinu ya kufanikisha uwekezaji ikiwemo usafiri wa barabara, anga, reli, nishati, upatikanaji wa maji safi na salama, maeneo ya uwekezaji na maboresho ya Huduma za Mahala Pamoja kwa wawekezaji kupitia ofisi ya TIC.