Home Biashara WAFANYABIASHARA WASHAURIWA KUTUNZA KUMBUKUMBU ILI KULIPA KODI STAHIKI

WAFANYABIASHARA WASHAURIWA KUTUNZA KUMBUKUMBU ILI KULIPA KODI STAHIKI

0

Mfanyabishara wa duka katika Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu
Paulina Hinda akichangia hoja wakati wa semina ya wafanyabishara
ambayo imeandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kufanyika
Mjini Nyashimo Wilayani humo.

*********************************

Na Veronica Kazimoto

Simiyu

Wafanyabiashara nchini wameshauriwa kutunza kumbukumbu za biashara
zao ili kulipa kodi stahiki na hatimaye kupunguza kero ya madai yao
kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inawakadiria kodi kubwa
isiyoendana na uhalisia wa biashara wanazofanya.

Akizungumza wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika
Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka
mamlaka hiyo Diana Masalla, amesema kuwa, wafanyabiashara walio
wengi hawana tabia ya kutunza kumbukumbu za biashara zao suala
linalosababisha malalamiko mengi baada ya kukadiriwa kodi na TRA.

“Ndugu zangu wafanyabiashara sote tunajua kwamba, mali bila daftari
hupotea bila habari hivyo basi, niwaombe mjenge tabia ya kutunza
kumbukumbu za biashara zenu siyo tu kwa ajili ya TRA lakini pia kwa ajili
yenu wenyewe kwani mtaweza kujua kama biashara zenu zinakua au
zinashuka lakini pia mtaweza kupanga bajeti za mauzo na manunuzi yenu
vizuri na mwisho wake mtalipa kodi stahiki na kuchangia maendeleo ya
nchi yetu,” amesema Masalla.

Masalla ameongeza kuwa, kuna tofauti kubwa kati ya mfanyabiashara
anayetunza kumbukumbu na yule asiyetunza kumbukumbu kwani
asiyetunza kumbukumbu kwa mauzo ya shilingi milioni 14 atalipa kodi
shilingi 450,000 kwa mwaka wakati anayetunza kumbukumbu kwa mauzo
hayo atalipa shilingi 320,000 kwa mwaka.

“Tukichukulia mfano wa wafanyabiashara wawili wenye mauzo ya shilingi
milioni 14, lakini mmoja anatunza kumbukumbu na mwingine hatunzi
kumbukumbu tunaona kwamba, kuna tofauti ya shilingi 130,000 kwa kuwa
asiyetunza atalipa shilingi 450,000 na anayetunza kumbukumbu atalipa
shilingi 320,000. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kutunza
kumbukumbu,” amesisitiza Masalla.

Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amewaambia wafanyabiashara hao
kuwa, nyenzo muhimu inayosaidia utunzaji wa kumbukumbu ni pamoja na
Mashine ya Kielektroniki ya Kutolea Risiti (EFD) na kama mfanyabiashara
hajafikia mauzo ya kutumia mashine ya EFD ambayo ni chini ya shilingi
milioni 14 anashauriwa kutumia kitabu cha risiti za kuandika kwa mkono
ambapo mfanyabiashara atakwenda na kumbukumbu hizo TRA kwa ajili ya
kukadiriwa kodi.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa mbao wilayani humo, Zakaria
Manyilizu amesema kuwa, elimu aliyoipata ya utunzaji kumbukumbu za
biashara ni nzuri hata hivyo ameiomba TRA kutoa elimu juu ya namna ya
kutumia mashine za EFD kwani walio wengi hawana utalaamu wa kutumia
mashine hizo.

“Kwa kweli tunaishukuru TRA kwa kutuletea elimu hii ya utunzaji wa
kumbukumbu hapa wilayani Busega lakini sisi tulio wengi hatujui kutumia
vizuri mashine za EFD hivyo ninaiomba TRA itufundishe namna ya kutumia
mashine hizi ili na sisi tunufaike na faida za utunzaji kumbukumbu
alizozieleza meneja wa TRA,” alisema Manyilizu.

Timu ya Maofisa wa kodi wakiongozwa na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi
Diana Masalla kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania wako Mkoani Simiyu
katika Wilaya ya Busega na Bariadi ambapo wanakutana na
wafanyabiashara mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi ikiwa ni
pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.