Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji
(wa pili kulia) akikabidhi tuzo ya Kampuni Bora DSE
kwa mwaka 2019 katika sekta isiyo ya Viwanda, kwa
Mkuu wa Uhusiano wa Uwekezaji na Miradi Maalumu
wa Vodacom Plc, Robin Kimambo. Kushoto ni Afisa
Mtendaji Mkuu wa DSE, Moremi Marwa na Afisa
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Usalama
wa Mitaji, Nicodemus Mkama. Hafla hii ilifanyika juzi
jijini Dar Es Salaam.
******************************************
Na Mwandishi Wetu
Kampuni inayoongoza kwa teknolojia ya mawasiliano
nchini Tanzania, Vodacom imeshinda tuzo ya soko la
Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Hafla ya kukabidhi tuzo hizo ilifanyika juzi jijini Dar es
Salaam, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni
‘Mazingira, Jamii na Utawala Endelevu’ Mgeni rasmi
alikuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Ashatu K. Kijaji.
Lengo kuu la tuzo hizi ni kukuza ubora wa biashara
katika nyanja ya Utunzaji wa Mazingira, Utawala Bora
wa Kampuni, Kuongeza Uwajibikaji katika shughuli za
Kijamii na kuhakikisha kuwa DSE inaendelea kutimiza
wajibu wake kwa wanachama.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa
Uhusiano wa Uwekezaji na Miradi Maalumu wa
Vodacom Plc, Robin Kimambo, alisema tuzo hiyo ni
heshima kubwa kwa kampuni hiyo ambayo kwa sasa
inaongoza kwa uvumbuzi kwenye teknolojia ya
mawasiliano nchini.
“Jambo la msingi ni kuwaahidi watanzania kuwa,
tutaendelea kuwa wabunifu na wavumbuzi ili kuendelea
kutoa huduma ambapo kwa sasa tuna takriban wateja
zaidi ya milioni 14 nchi nzima,” alisema.
Washiriki wa tuzo hizo ni kampuni zilizoorodheshwa
DSE ambazo ni pamoja na Madalali au
Wafanyabiashara, Washauri waliopendekezwa pamoja
na vyombo vya habari vya kidigitali na magazeti.
Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc iliorodheshwa
katika Soko la Hisa la Dar es Salaam Agosti 15, 2017.