Home Mchanganyiko WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI KWA MABORESHO YA FIDIA KWA WAFANYAKAZI NCHINI

WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI KWA MABORESHO YA FIDIA KWA WAFANYAKAZI NCHINI

0

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist Ndikilo akitoa maelekezo alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Pwani.

Afisa Uwekezaji Mwandamizi Bw. Michael Semiono akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist Ndikilo alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Pwani.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist Ndikilo akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Pwani. .

Afisa Uwekezaji Mwandamizi Bw. Michael Semiono akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist Ndikilo machapisho ya WCF alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Pwani.

…………………………..

Na. Sarah Reuben

Wananchi waliotembelea Maonesho ya Pili ya Viwanda mkoani Pwani wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maboresho makubwa ya fidia kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na umma. 

Akizungumza alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist Ndikilo amesema tangu kuanzishwa kwake Mfuko huu umekuwa faraja kwa wafanyakazi wengi hususan wafanyakazi wa viwandani.

“Binafsi niwapongeze sana WCF kwa kuwa mnafanya kazi nzuri sana na hata wananchi wameendelea kuipongeza sana Serikali kwa kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii hususan malipo ya fidia kwa wafanyakazi. Hali hii imechangia kuongeza motisha kazini na  kuimarisha mahusiano kati ya mwajiri na wafanyakazi wake,” alisema Eng. Ndikilo.

Eng. Ndikilo aliwaalika wananchi kutembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ili kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya Mfuko huo ikiwemo taratibu za madai ili kuepukana na usumbufu unaoweza kujitokeza pindi mfanyakazi atakapopata ajali, ugonjwa au kifo kutokana na kazi. 

Nao baadhi ya wajiri walipotembelea banda la WCF wamesema wameongeza uelewa kuhusu masuala ya fidia na mafao yanayotolewa na WCF. 

“Mimi binafsi nilidhani bima ya afya inagharamia matibu yoyote ya mgonjwa hata yale yanayotokana na ajali au ugonjwa unaotokana na kazi lakini leo nimefahamu WCF ndiye mwenye kulipa gharama za matibabu hayo,” alisema Dkt. Aden Mpangile alipotembelea banda la Mfuko huo. Aliongeza kuwa, “Hapo awali sikufahamu kuwa kiwango cha fidia anachostahili kulipwa mfanyakazi hujulikana baada ya tathmini kufanyika kwa mfanyakazi aliyekamilisha huduma za matibu ambayo kimsingi matibabu hayo hugharamiwa na Mfuko”. 

Naye Afisa Uwekezaji Mwandamizi Bw. Michael Semiono amesema WCF ni mdau mkubwa wa maonesho ya viwanda ndio sababu Mfuko umeamua kushiriki kwenye maonesho haya ili kukutana na wadau wake ikiwemo wafanyakazi na wamiliki wa viwanda nchini. Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda, Mfuko umejielekeza kwenye miradi ya viwanda nchini iliyopo mkoa wa Dodoma, Morogoro, Tanga na Simiyu alisema Afisa huyo.  

Kuhusu mafao yatolewayo na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Semiono amesema Mfuko unatoa mafao kadha wa kadha ikiwemo huduma ya matibabu yanayotolewa kwa mfanyakazi aliyepata ajali au ugonjwa utokanao na kazi. Aliongeza kuwa Mfuko hugharamia huduma za ukarabati na ushauri nasaha pamoja na malipo ya ulemavu wa muda au ulemavu wa kudumu kwa mfanyakazi aliyekamilisha matibabu na kugundulika ana ulemavu huo.

Mafao mengine ni malipo kwa mtu anayemhudumia mgonjwa iwapo daktari watathibitisha mfanyakazi aliyepata ajali au ugonjwa kazini hawezi kujihudumia, msaada wa mazishi na malipo kwa wategemezi iwapo mfanyakazi atafariki kutokana na kazi. 

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi unashiriki kwa mara ya pili kwenye maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wadau wengi zaidi ili kutoa elimu kuhusu taratibu za madai kwa mfanyakazi aliyepata ajali, ugonjwa au kifo kutokana na kazi pamoja na majukumu ya Mfuko kwa ujumla. 

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni Taasisi ya Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambao umeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na. 20 ya mwaka 2008.