Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Watumishi wa sekta ya ardhi wa halmashauri za Wilaya na Mji za mkoa wa Geita jana wakati wa ziara yake ya kuangalia utendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Geita.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua Mradi wa ujenzi wa Ofisi na Nyumba za Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Chato mkoa wa Kagera wakati akikagua miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Chato Charles Kabeho na kulia kwa Naibu Waziri ni Mhandisi wa ujenzi wa Mradi huo Renatus Mhada.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Chato mkoa wa Kagera Charles Kabeho akielekea kukagua Mradi wa ujenzi wa Ofisi na Nyumba za Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Chato mkoa wa Kagera wakati akikagua miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
……………………..
Na Munir Shemweta, WANMM GEITA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinalinda maeneo yote ya hifadhi yaliyoidhinishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kuwa vijiji ili yasiendelee kuvamiwa.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na watendaji wa sekta ya ardhi wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Geita wakati wa ziara yake ya siku moja kutembelea mkoa huo kuangalia utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kufuatia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa mwezi Machi 2019.
Alisema, ni jukumu la halmashauri za wilaya wakati zikisubiri kuletewa tarifa rasmi ya maeneo yaliyoidhinishwa kuwa vijiji na mengine yaliyobadilishiwa matumizi kuyalinda maeneo hayo yasivamiwe tena ili taarifa itakapokwenda katika halmashauri husika kuhusiana na maeneo pasiwepo uvamizi mwingine zaidi ya ule wa awali kabla ya kutembelewa na timu ya Mawaziri nane.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, halmashauri ambazo maeneo yake ya hifadhi yalivamiwa na vijiji vyake kuidhinishwa zitapelekewa taarifa sambamba na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali vijiji vilivyidhinishwa.
‘’Mna jukumu kulinda maeneo hayo yasivamiwe tena kwa sababu kamati ya mawaziri wanne walipita kwenye baadhi ya maeneo na yaliainishwa na kinachotakiwa kwenu ni kuhakikisha hakuna uvamizi unaoendelea katika hifadhi ’’ alisema Dkta Mabula.
Alisema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ishamaliza kupanga maeneo ya vijiji yaliyoidhishwa mkoa kwa mkoa na kinachofanyika sasa ni kutangazwa katika Gazeti la Serikali ili wananchi waweze kuishi kwa amani katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dorothy Mwanyika wakati wa kikao hicho na watendaji wa sekta ya ardhi alisema wizara yake katika kukabiliana na upungufu wa watumishi wa sekta hiyo imejipanga kuhakikisha inawagawa watumishi wa sekta ya ardhi waliopo katika halmashauri kulingana na idadi iliyopo sasa.
Mwanyika alisema Wizara ya Ardhi ina mahitaji ya watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri zote wapatao 2900 ambapo kwa sasa kuna jumla ya watumishi 1500 hivyo kufanya kuwepo pungufu ya watumishi 1400. Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi alisema, kinachofanyika sasa sasa kwa Wizara yake ni kutambua watumishi waliopo na baadaye kuwatawanya katika mgawanyo mzuri.
Naye Kamishna Msaidzi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo alisema halmashauri ambazo hazina wataalamu wa kutosha zinazoazima kutika mikoa iliyo jirani na halmashauri hizo wataalamu wake wa sekta ya ardhi wanatakiwa kufanya kwa weledi na si vinginevyo ili kazi ya sekta hiyo iweze kwenda vizuri.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Ofisi na Nyumba za Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) uliopo wilayani Chato mkoani Kagera.
Akiwa katika ukaguzi wa mradi huo unaogharimu Bilioni 1.2 na kusimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt Mabula alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuhakikisha linakamilisha ujenzi wa mradi huo katika muda uliopangwa kwa kuwa shirika hilo sasa limeamiwa na serikali kwa kupatiwa miradi mbalimbali nchini.