Na, Farida saidy,Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare amewataka Viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Gairo Mkoani humo kufanya kazi na watumishi wao kwa karibu, Usawa na bila kuweka matabaka ili kuimarisha Umoja miongoni mwao.
Mhe. Ole Sanare ametoa Maagizo hayo Oktoba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo alipofika Wilayani hapo kwa lengo la kuwasalimia na kujitambulisha akiwa njiani kutoka Dodoma kikazi.
Mhe. Sanare alipata fursa ya kuongea na watumishi wa Halmashauri hiyo na kubainisha kuwa hadi sasa amekwishapokea ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa wananchi na watumishi wakieleza kuwa mambo hayako shwari ndani ya Halmashauri hiyo, hivyo akawataka viongozi kutoweka matabaka katika utendaji wao wa kazi.
“wasaidie waweze kufanya kazi zao vizuri, tusije tukajaribu kuwa na matabaka ndani ya utumishi” alisema Mhe. Sanare.
Aidha, Mhe Sanare amekemea tabia ya kutumia fedha za makusanyo ya ndani ya halmashauri kabla hazijaingizwa kwenye Ankauti ya Benki ya Halmashauri hiyo, na kwamba huo sio utaratibu wa Serikali, hivyo ameagiza matumizi yote ya fedha za makusanyo ya ndani ya halmashauri hiyo yafanyike baada ya fedha hizo kuingizwa kweny Ankaunti ya Benki ya Halmashauri.
“Kuanzia leo fedha zote ziingie kwenye Ankaunti ya Halmashauri zitoke kwenye Ankaunti kwa ajili ya matumizi”alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Sambamba na hayo Mhe. Ole Sanare ameomba ushirikiano kutoka kwa watumishi wa Halmashauri hiyo, kushirikiana na Ofisi yake pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya ili kuondoa sintofahamu iliyopo katika Halmashauri hiyo.
“Nini hiki kinachoedelea ndani ya Halmashauri, hatupaswi kuvumilia hata dakika moja. Mlango ulioingilia ndio huu utatokea huo huo”. alionya.
Amesema anajua kuna mambo ya ovyo yanaendelea kufanyika katika Halmashauri hiyo, hata hivyo amewahakikishia kuwa mambo hayo yapo mwishoni kuisha na kwamba itabidi kuvumilia pale atakapolazimika kuchukua hatua za kinidhamu kwa baadhi ya watumishi wa Umma wasiowajibika ipasavyo.
Pamoja na kutoa onyo hilo kwa watumishi wanaofanya kazi ndani ya Halmashauri hiyo bado amewapongeza watumishi ambao wanaendelea kufanya kazi zao kwa bidii, uadilifu na uwajibikaji mkubwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Masasi Kalobelo ameungana na Mkuu wake wa Mkoa, kutaka viongozi wa Halmashauri hiyo kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia matumizi yake.
Mhandisi Kalobelo pia amesema usimamizi wa miradi ya maendeleo bado ni changamoto kwa Halmashauri hiyo na kwamba ataomba kupewa taarifa ya miradi yote ikiwemo miradi yenye changamoto katika utekelezaji wake aliyoiita Miradi chechefu ili aifanyie kazi.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo ameagiza watendaji wa Halmashauri hiyo kutoa taarifa mbalimbali za Kiserikali katika Ofisi yake kwa wakati na zilizo sahihi.
“kitu ambacho ni kipimo cha ufanyakazi wetu na ufanisi wetu ni utoaji wa taarifa kwa wakati na iliyosahihi” alisema Mhandisi Kobelo.
“kwamba tunapaswa kufikia lengo, lengo halifikiwi katikati kumekuwa na sababu lakini inawezekana sababu zimekuwa hazitolewi kwa wakati” alisisitiza.
Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa amewataka watumishi wa Serikali katika Wilaya hiyo na Mkoa mzima kwa jumla kusimamia kwa ukamilifu zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa linalotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Siriel Mchembe alimueleza Mkuu wa Mkoa mwelekeo mzuri wa makusanyo ya ndani ya mapato ya Halmashauri hiyo kutokana na uwepo wa machimbo ya madini ya Dhahabu ya Kilama huku akiomba mahusianao baina ya Ofisi yake na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuboreshwa.
Nao watumishi wa Halmashauri hiyo wamemueleza Mkuu wa Mkoa changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo changamoto ya kukosekana kwa UMOJA miongoni mwao.
Hivyo, Wamemuomba Mkuu wa Mkoa kuitolea ufumbuzi changamoto hiyo kwani licha ya changamoto hiyo kuwawacheleweshea wananchi maendeleo yao lakini pia ni kikwazo kwa watumishi wa Wilaya hiyo katika Utendaji wao wa kazi.