Naibu Spika Dr. Tulia Ackon kwa kushirikiana na taasisi yake ya Tulia Trust amefanya ziara katika Shule ya Sekondari Ivumwe iliyopo mkoani Mbeya ambapo ametoa msaada wa Shilingi Milion mbili na laki tano (Tsh. 2,500,000/-) aliyokuwa ameahidi katika shule hiyo ili kusaidia uboreshaji wa miundombinu katika shule hiyo ikiwemo uchakavu wa madarasa, maabara pamoja na bweni la watoto wa kike.
Aidha, Dr. Tulia amesisitiza kwamba kupitia taasisi hiyo ya Tulia Trust ambayo inajikita katika kusaidia sekta mbalimbali nchini ikiwemo Elimu na Afya ataendelea kutoa misaada mbalimbali katika Shule ikiwa ni sehemu ya kushiriki kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.
Akizungumza na Wanafunzi wa Shule hiyo Dr. Tulia amesema “Mimi nimetembelea shule nyingi sana hapa nchini, watoto wa shule hii ya Ivumwe mazingira yenu ni mazuri mno ukilinganisha na shule nyingine, kwamaana hiyo hakuna sababu yoyote ya kufeli, natamani sana kuzisikia hadhithi nzuri za ufaulu. Niwaombe sana watoto wazuri msome kwa bidii ili muweze kulisaidia taifa, hata mimi hapa mnaponiona na huu Udaktari wangu sio kanakwamba nimepewa tu, hapana, ni Udaktari wa kisomo hivyo na nyie mkazane kusoma ili kutimiza ndoto zenu”-Dr. Tulia
Katika hafla ya kukabishi fedha hizo Diwani wa Kata ya Mwakibete Lucas Mwampiki (CHADEMA) amesema maendeleo hayana itikadi hivyo anampongeza Dr. Tulia kwa kuchangia maendeleo katika Kata yake kwani ni mara ya tatu sasa Naibu Spika anachangia shughuli za maendeleo katika Kata hiyo. “Nakushukuru Naibu Spika kwa shughuli unazozifanya kwani katika shule hii inayosimamiwa na CCM mimi nina ndugu zangu 52 wanaosoma hapa na sifa inayopatikana ni ya Mwakibete na Mbeya kwa ujumla” alisema Mwampiki