Home Mchanganyiko WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI ASEMA NISHANI...

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI ASEMA NISHANI ALIYOPEWA DKT SALIM ANASTAHILI

0

Watanzania wametakiwa kuyafanya majukumu ya kitaifa wanayopewa na viongozi wa serikali kwa uzalendo usiotiliwa mashaka,uamini na ufanisi kama walivyoelekezwa wakati wa kukabidhiwa majukumu hayo kwa faida ya Nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi wakati akitoa Kongole kwa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim kufuatia kitendo cha kukabidhiwa Nishani ya Juu ya Urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China nishani ambayo inamfanya Dkt. Salim kuwa mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya China.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa nishani aliyokabidhiwa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim imeliletea heshima kubwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nay eye mwenyewe kutokana na utendaji wake usiotiliwa mashaka baada ya kuaminiwa na kukabidhwa majukumu hayo na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuwataka Watanzania wote hususani vijana kuiga mfano huo.

Amesema Dkt Salim Ahmed Salim ni Mtumishi mwaminifu na mzalendo kwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameitumikia nchi katika nafasi mbalimbali kuanzia na ukurugenzi katika wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki balozi katika nchi za Misri,India,China na Umoja wa Matifa lakini pia ,Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Waziri wa Mambo ya Nje,Naibu waziri Mkuu kisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadae  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

 Nishani hiyo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping ilipokelewa na Bi. Maryam Salim, Binti ya Dk. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Albania kwa niaba ya Baba yake kutokana na kushindwa kuhudhuria kwa sababu za kiafya. 

Katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania iliwakilisha na Balozi wa Tanzania nchini China Mheshimiwa Mbelwa Kairuki.

Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya kukabidhi nishani ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ya China akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Wang Qishan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang, Spika wa Bunge Mheshimiwa Li Zhanshu na Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza la Taifa. 

Nishani ya Juu ya Urafiki ya Taifa la China imetolewa kwa Dkt. Salim  kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.  

Aidha, mchango wa Dk. Salim katika kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania wakati aliposhikilia nyadhifa mbalimbali umetajwa kama sababu ya kutunukiwa Nishani hiyo. Vilevile, mchango wa Dk.Salim katika kujenga mahusiano kati ya China na Afrika akiwa na nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU umetajwa kuwa sababu nyingine ya kutunukiwa Nishani.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini China Balozi Mbelwa Kairuki amesema mamilioni ya Wachina hususani vijana wamepata fursa ya kufahamu nafasi na mchango wa Tanzania na Bara la Afrika katika historia ya taifa lao.

 Aidha, tukio la leo limeifanya Tanzania kufahamika kwa watu wengi zaidi nchini China kupitia tukio mara moja. Hatua hiyo itaamsha udadisi na hamasa miongoni mwa Wachina wengi wa kizazi kipya kutaka kuifahamu zaidi Tanzania. Hali hii yaweza kujitafsiri katika fursa kubwa ya kukua kwa utalii, biashara na wawekezaji ikizingatiwa kuwa  wananchi wa China hutoa mwitikio mkubwa kwa nchi ambazo husemwa vizuri na kuthaminiwa na Serikali yao.

Ni kwasababu hiyo, katika maadhimisho ya miaka 70 ya Taifa la China, Jumuiya ya Urafiki wa watu wa China na Tanzania ni miongoni mwa Jumuiya za mataifa 17 yenye urafiki wa majira yote na China walioalikwa  kushiriki kwenye maadhimisho hayo na tarehe 1 Oktoba 2019 watakuwa na gwaride lao maalum. Katika jumuiya hizo 17,  Kutoka Barani Afrika ni Tanzania na Zambia ndio watahudhuria.