Na Dotto Mwaibale, Singida
NCHI sita za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) kushiriki maonesho ya pili ya viwanda vidogo vidogo (SIDO) kitaifa 2019 mkoani Singida.
Nchi zitakazo shiriki maonesho hayo ni Kenya, Burundi, Ruanda, Uganda, China, India na Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (pichani) alisema maonesho hayo yataanza kufanyika Oktoba 4 hadi 9 mwaka huu.
” Maonesho haya yatafanyika sanjari na maadhimisho ya wiki ya chakula duniani ambayo yatafanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 16 mwaka huu katika Viwanja vya Bombadier zamani Peoples” alisema Nchimbi.
Nchimbi alisema kufanyika maonesho hayo mkoani Singida ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo ambao unakuwa kiuchumi kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, biashara na viwanda.
Alisema Mkoa wa Singida wanajivunia kuchaguliwa kufanyika kwa maonesho hayo kitaifa na hii itawapa hamasa kubwa wananchi katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya usindikaji kutokana na mazao yanayolimwa mkoani hapa pamoja na vya mafuta ya alizeti.
Dkt. Nchimbi alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi wote wa mkoa wa Singida kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo.