MTANZANIA PEKEE KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA YA MASHUA ZA UPEPO , SEPT 2019

  0

  Nassoro Mahruki akiwa kazini katika mashua ya Zhuhai yenye mabaharia toka
  mataifa China, Marekani, Uingereza, Canada, Ufaransa, nk

  Moja ya majengo ya mandhari ya hoteli Mnarani , Nungwi kaskazini ya Zanzibar. Bw
  Mahruki ameendesha biashara za utalii, Zanzibar na Pemba kwa miaka 23 sasa. Ni mtu anayependa kazi na shughuli azifanyazo. Mchapa kazi na Mjasiria Mali wa mfano.

  Nassoro Mahruki akiwa na nahodha wa mashua husika (“Zhuhai”), Nick Leggatt,
  mzawa wa Afrika Kusini mwenye uzoefu wa muda mrefu. Keshazunguka dunia kwa
  mashua hizi mara tatu!

  *************************

  Picha na Habari za Freddy Macha

  Wangapi tumewahi kusikia mashindano ya kimataifa ya mashua za upepo (“clipper
  race” )? Mimi sikuyajua hadi nilipomhoji Nassoro Mahruki, Mzanzibari mshiriki wa
  tukio hilo litakalochukua miezi kumi na moja hadi Agosti 2020.

  Nassoro Mahruki ambaye huendesha shughuli zake za biashara za utalii visiwani
  Pemba na Unguja, ni Mwafrika Mashariki pekee na anasema alijitayarisha kwa
  miaka miwili kushiriki.

  “Yakubidi ufanye mafunzo na kufaulu …” alisema akinionyesha mashua iitwayo
  “Zhuhai” ikiongozwa na nahodha Nick Leggatt. Zhuhai ni kati ya vyombo vingine
  kumi na moja vyenye majina kama “Korea”, “Punta Del Este”, “WTC Logistics”, nk.

  Dimba hili lilianzishwa hapa London mwaka 1996. Mwasisi wake, aliyeshatunukiwa
  heshima ya “Sir” na Malkia Elisabeth wa Uingereza ni Robin Knox Johnson. Bw
  Johnson alikuwa mwanadamu wa kwanza kuzunguka dunia nzima kwa mashua
  inayotegemea upepo tu mwaka 1968. Keshafundisha zaidi ya mabaharia 5,000.

  Kitatange hiki kinahusu kila aina ya changamoto za kimichezo. Kushirikiana na
  wenzako, dhoruba zenye pepo kali, mvua, barafu, mawimbi nk. Usafiri ulioanzia
  London Septemba Mosi , 2019 utapitia mabara yote na bahari kubwa zaidi ya sita,
  Ureno, Uruguay, Afrika Kusini, Australia, China, Marekani, visiwa vya Bermuda,
  Panama, nk. Watarejea London Agosti 2020. Nilipowasiliana naye leo alikuwa tayari
  salama Ureno.

  Nassoro Mahruki aliyevalia bendera za Tanzania, Zanzibar, Pemba alisema mbali ya
  kupenda michezo ya majini lengo ni kujenga tasnia ya utalii wa majini Tanzania.

  “Ikiwa washindani wenzangu wako radhi kununua meli ya paundi milioni kumi,
  hawatashindwa kuja Tanzania kuchezea maji na kutumia dola elfu mbili kwa juma.
  Ni hela nzuri sana kwa utalii wetu.”

  Mataifa zaidu ya 40 yamo mwaka huu na Afrika ina nchi nne tu : Tanzania, Nigeria,
  Misri na Morocco.

  Tumpe heko na kumwombea dua arejee salama. Fahari yetu.