Home Mchanganyiko TAASISI YA TIA KUBORESHWA KUENDANA NA MPANGO WA MIAKA MITANO

TAASISI YA TIA KUBORESHWA KUENDANA NA MPANGO WA MIAKA MITANO

0

Mhadhiri wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Bw. Burkadi Haule, akitoa ufafanuzi wa ramani ya majengo ya taasisi hiyo, katika maeneo mbalimbali nchini, kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, wakati wa ziara ya kutathimini utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2018/19, jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, akieleza nia ya Wizara ya Fedha na Mipango ya kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha
miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania-TIA, ili kwenda sambamba na lengo la Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano.

Mtaalam wa masuala ya Sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Msabaha
Msabaha, akihoji kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2018/19 na changamoto zake, wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Khatibu Kazungu (hayupo pichani), katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania- TIA- jijini Dar es Salaam.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya TIA, Bi. Luciana Hembe (kushoto) na
Mhadhiri wa taasisi hiyo, Bw. Burkadi Haule, wakisikiliza maagizo ya Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (hayupo pichani), katika Taasisi ya TIA, jijini Dar es Salaam

Baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania- TIA- jijini Dar es Salaam
wakisikiliza maelezo ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt.
Khatibu Kazungu (hayupo pichani), kuhusu kufanya kazi kwa weledi na maadili kwa ajili ya maendeleo ya Taifa

Moja ya ramani ya majengo ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania- TIA, ambayo yanatakiwa kujengwa ili kuwezesha upatikanaji wa wahasibu wakutosha kulingana na mpango wa maendeleo wa miaka mitano. (Picha na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam)

********

Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam

Serikali imeahidi kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya
Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) ili kuongeza udahili wa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa wahasibu wa kutosha kama mpango wa Taifa wa miaka mitano ulivyoelekeza.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipang,o Dkt. Khatibu Kazungu, wakati wa ziara yake ya kikazi katika taasisi hiyo iliyochini ya Wizara ya Fedha na Mipango kubaini changamoto za utekelezaji wa Bajeti ya taasisi hiyo kwa mwaka 2018/19.

Dkt. Kazungu alisema kuwa Taasisi ya TIA inakabiliwa na changamoto kubwa ya ufinyu wa bajeti jambo lililosababisha baadhi ya miundombinu yake kutokamilika kwa wakati na hivyo kupunguza kiwango cha udahili wa wanafunzi.

“Lengo la Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano ni pamoja na taifa
kuzalisha wahasibu wa kutosha ili kuleta chachu katika maendeleo ya uchumi na nyanja zingine za maendeleo, malengo yanayotegemewa kwa kuimarishwa kwa miundombinu ya taasisi hii”, alieleza Dkt. Kazungu

Alisema kuwa miundombinu inayoangaziwa kwa mwaka huu wa fedha ni pamoja na Mabweni ya wanafunzi, vyumba vya madarasa na ofisi za watumishi, aidha kuangalia uwezekano wa kuongeza wahadhiri kulingana na kozi zinazotolewa jambo litakalokwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji wa Taasisi ya TIA Bi. Luciana Hembe, alieleza kuwa, hatua ya viongozi wa juu kutembelea taasisi wanazoziongoza na kuona uhalisia wa mambo, unaongeza morali ya kiutendaji ya watumishi kwa kuwa hutatua changamoto nyingi hususani za kibajeti.

Alisema kuwa Taasisi ya TIA imejipanga kikamilifu kuhakikisha wahitimu wake
wanakuwa na weledi wa kutosha katika kuhimili ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi.