*************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka benki ya NMB vyenye thamani ya sh. milioni 25.
Vifaa hivyo ni fremu 46 za madirisha ya alminium na vioo vyake, milango 18, mabati 56, misumari na mbao, kompyuta 10, madaftari 4,050 vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 25/-.
Akipokea msaada huo leo mchana (Jumapili, Julai 28, 2019) kwenye zahanati ya Nandagala, wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu amewashukuru viongozi wa benki hiyo kwa kuamua kuchangia vifaa hivyo.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nandagala, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, amesema mchango uliotolewa unamaanisha kazi ya kukamilisha jengo la wodi ya wagonjwa na vyumba vya madaktari ni lazima ifanyike haraka.
“Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NMB kwa msaada huu mkubwa. Hii maana yake ni kwamba ni lazima tuharakishe kukamilisha jengohili ili tuanze kutoa huduma kwa wananchi wa Nandagala na wa vijiji vya jirani,” alisema.
“Tulianza na ujenzi wa zahanati kisha tukajenga jengo la upasuaji lenye wodi mbili. Moja ya wanaume na nyingine ya wanawake ambazo kila moja ina uwezo wa kulaza wagonjwa 20 kwa wakati mmoja.”
Jengo hili jipya ambalo tumelianza ujenzi wake, likikamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 60. Pia kuna jengo lenye vyumba vya madaktari, vyumba vya upasuaji na vyumba vya kujifungulia.
Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao wafikirie uwezekano wa kujenga wodi nyingine na pamoja na jiko ili wagonjwa watakaokuwa wanalazwa hapo, wapate mahali pa kupikiwa chakula.
Mapema, akitoa taarifa ya msaada huo, Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali katika benki ya NMB, Bi. Vicky Bishubo alisema kipaumbele cha benki hiyo kila mara ni kutatua changamoto za afya na elimu kwani sekta hizo ni nguzo kuu ya maendeleo kwa Taifa lolote.
“Vitu hivi (mabati, madirisha ya aluminium, kompyuta na madaftari) tunavyokabidhi leo ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii na sisi kama benki inayoongoza Tanzania tunahakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika kutokana na faida tunayoipata,” alisema.
Alisema kwa mwaka huu, NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu. “Mpaka ninavyoongea leo, tayari tumetoa misaada yenye thamani ya zaidi ya millioni 600 kwa mwaka huu wa 2019 tu,” alisema.
Akielezea kuhusu programu ya WAJIBU, Bi. Bishubo alisema hadi sasa wameshawafikia vijana wasiopungua 42,000 katika shule za msingi na sekondari kwa kuwapa elimu ya fedha na kujifunza kuweka akiba katika umri mdogo kupitia programu yake ya ‘Jifunze, Jipange na Wajibika’ (WAJIBU).
“NMB imekuwa ikiwawezesha vijana kupata elimu ya fedha katika shule za msingi na sekondari Tanzania. Elimu hii ya fedha kwa vijana hutolewa na wafanyakazi wetu wa benki kwenye shule zilizopo karibu na benki ikilenga kuwafundisha vijana umuhimu wa kuweka akiba na mipango kwa ajili ya maendeleo yao na kukidhi mahitaji ya muhimu,” alisema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nandagala, Bw. Andrew Chikongwe aliishukuru benki hiyo kwa kuwasaidia vifaa hivyo ambavyo alisema vimefika kwa wakati muafaka. “Majengo yalikwishakamilika, yakabakia madirisha na milango, pamoja na vifaatiba, kwa hiyo sasa hivi tunaweza kuendelea na ujenzi,” alisema.