Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbwamaji uliopo Gezaulole Kata ya Somangila Wilayani Kigamboni, Yohana Luhemeja akiwa kwenye eneo hilo la jengo la kisima.
Mkimbiza Mwenge akimtwisha na kumtua ndoo ya maji mmoja wa akina mama wa Gezaulole kama ishara ya kuzindua mradi wa maji Kisima cha Gezaulole. (Picha na Andrew Chale).
…………………
Na Andrew Chale, Kigamboni
WANANCHI wa Mtaa wa Mbwamaji uliopo Gezaulole Kata ya Somangila Wilayani Kigamboni wamempongeza Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo Yohana Luhemeja kwa juhudi zake za kusimamia maendeleo ikiwemo suala la upatikanaji wa maji safi na salama.
Wananchi hao wametoa pongeza hizo mapema jana Julai 23 wakati wa Mwenge wa Uhuru uliotembelea kukagua mradi huo ambao utasaidia wakazi zaidi ya 8000 Mtaa huo wa Mbwamaji, Somangila.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye tukio hilo la Mwenge wa uhuru uliotembelea kukagua mradi huo, Wananchi hao walieleza kuwa maendeleo hayana Chama na kwa hatua na juhudi za Mwenyekiti alizoahidi awali miaka kadhaa iliyopita zimeweza kutimia.
“Awali mradi huu ulikufa na hakukuwa na mtu mwenye kutaka kuonesha nia ya kuufufua, tunashukuru Mwenyekiti wa Serikali wetu licha ya kutoka upinzani alipoingia kushika nafasi hii alianza na suala la hiki kisima na kwa kushirikiana na kamati yake waliweza kuonesha juhudi na hatua zimechukuliwa na sasa kisima kimefufuliwa. Hizi ni juhudi kubwa tunawapongeza wote ikiwemo Dawasa na viongozi wa Halmashauri kwa pamoja kwa kumuunga mkono” alieleza Sagala Msumi mkazi wa Mbwamaji.
Nao baadhi ya Wanawake wa Mtaa huo akiwemo Ester Modest na Falhaty Mussa wameshukuru kwa hatua hiyo kwani kwa sasa kero ya maji itakuwa ni historia kwao ambapo walikuwa wakikumbwana na changamoto ya maji safi na salama ya matumizi ya nyumbani.
“Tumekuwa tukitumia maji ya visima ambavyo baadhi yake sio salama hivyo kukamilika kwa kisima hiki kitatusaidia sana tunamshukuru sana Mwenyekiti wetu na Kamati yake kwa ujumla”alieleza Bi. Ester Modest.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo Yohana Luhemeja ameeleza kuwa, mradi huo wa kisima hicho utaenda kusaidia Wananchi kwenye zaidi ya Kaya 8000 na kwa sasa tayari mabomba yanaendelea kutandikwa ardhini na mwezi Desemba mwaka huu maji yataanza rasmi.
“Kisima hiki ni cha muda mrefu na kwa sasa kimefufuliwa na kipo tayari kwa kuanza kazi kwani wananchi wameanza kusambaziwa mabomba pia mitaa mitatu itaenda kunufaika na maji haya kuanzia Mwezi Desemba mwaka huu” alisema Mwenyekiti huyo.
Yohana Luhemeja aliongeza kuwa: mradi huo wa kisima hicho awali ulikuwa wa Kijiji cha Gezaulole lakini ukafa na kubaki bustani pekee hata hivyo katika moja ya ahadi zake wakati wa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo ya Uenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliahidi kufufua kisima hicho na kwa sasa ahadi imetimia huku akiwapongeza DAWASA
na Halmashauri ya Kigamboni kwa kuweza kumuunga mkono kwenye suala hilo la kukifufua na kwa sasa wananchi wa Gezaulole watapata maji ya uhakika.” Alimalizia Mwenyekiti huyo, Yohana Luhemeja.
Aidha, Mwenge huo wa Uhuru katika Wilaya hiyo ya Kigamboni umeweza kutembelea na kukagua miradi 5 yenye thamani ya Bilioni 14, ikiwemo kisima hicho cha Maji Gezaulole.