Home Mchanganyiko KUFIKIA JULAI 30 WAKULIMA WOTE WATAKUWA WAMELIPWA FEDHA ZA PAMBA-MHE HASUNGA

KUFIKIA JULAI 30 WAKULIMA WOTE WATAKUWA WAMELIPWA FEDHA ZA PAMBA-MHE HASUNGA

0
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mzani wa kupimia Pamba mara baada ya kuwasili katika kijiji na kata ya Nyamigota Halmashauri ya Mji wa Katoro kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu sintofahamu kwenye zao la Pamba wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita, Jana tarehe 18 Julai 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua kiwanda cha kuchakata pamba kilichotelekezwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) kilichopo Wilayani Mbogwe wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita, Jana tarehe 18 Julai 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara kutoa ufafanuzi kuhusu zao la Pamba mara baada ya kuwasili katika kijiji na kata ya Msasa, wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita, Jana tarehe 18 Julai 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akimsikiliza kwa makini Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko kabla ya kuzungumza na wakazi wa Kijiji cha Namparahala kilichopo katika kata ya Busonzo katika wilaya ya Bukombe Mkoani Geita wakati wa mkutano wa hadhara kutoa ufafanuzi kuhusu zao la Pamba, Jana tarehe 18 Julai 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo mbele ya kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya ya Mbogwe wakati akitoa ufafanuzi kuhusu zao la Pamba, wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita, Jana tarehe 18 Julai 2019.
 
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Geita
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa hadi kufikia Julai 30, 2019 wakulima wote wa Pamba nchini watakuwa wamelipwa.
Hivi karibuni kumetokea hali ya sintofahamu kuhusiana na suala ununuzi wa zao hilo baada ya kutangazwa kwa bei elekezi ambayo ni sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.
Alisema kuwa miongoni mwa changamoto za wanunuzi ni dhamana ya serikali katika taasisi za kifedha. Ambapo tayari serikali imeridhia kuwadhamini ili kununua zao hilo.
Waziri Hasunga ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Julai 2019 wakati akizungumza kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Wilaya ya Mbogwe, Bukombe na Geita wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Mhe Hasunga alisema kuwa Serikali imeamua kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la pamba kutokana na kusuasua kwa soko lake kwa kutoa dhamana ili kuwawezesha wanunuzi kukopeshwa fedha na benki mbalimbali kwa ajili ya kununulia pamba kutoka kwa wakulima.
   
Wakati huo huo Mhe Hasunga aliwasihi wakulima wa zao hilo la pamba na wakulima wa mazao mengine nchini wahakikishe mara baada ya kuuza mazao yao wanatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia pembejeo watakazozitumia katika msimu ujao.
“Pamoja na kwamba mtalipwa fedha nzuri iliyopangwa na serikali ya shilingi 1200 lakini nawakumbusha kuwa serikali sasa haitawakopesha pembejeo hivyo ni vyema mkatenga fedha ili kununua pembejeo hizo” Alikaririwa Mhe Hasunga
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alisema Serikali itahakikisha inaendelea kutafuta masoko ya mazao hayo ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa masoko kwa mazao yao na hivyo kujiongezea tija.
Pia, alisema mbali na kutafuta masoko, Serikali imedhamiria kufufua viwanda mbalimbali vya nguo hapa nchini ili kuwawezesha wakulima wa zao la pamba kuwa na soko la uhakika.
“Kuhusu suala la maghala tunatambua tatizo hilo na tutahakikisha tunayaboresha ili pamba iweze kuhifadhiwa katika mazingira bora” Alisema
Akizungumzia kuhusu changamoto ya viuatilifu, Waziri Hasunga alisema Serikali itahakikisha vinapatikana kwa kuzingatia eneo husika ili kuweza kudhibiti wadudu waharibufu.
Sambamba na hayo Mhe Hasunga ametoa miezi miwili kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) kuhakikisha
kuwa kinafufua kiwanda cha kuchakata Pamba Kilichopo katika Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita na kufikia mwaka 2020 kianze kufanya kazi.