Home Mchanganyiko SERIKALI KUOKOA BILIONI 25 KIGOMA ZA KUZALISHA UMEME

SERIKALI KUOKOA BILIONI 25 KIGOMA ZA KUZALISHA UMEME

0

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akisaini kitabu cha wageni katika kituo cha kuzalisha umeme, alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi  katika kituo hicho.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu,( katikati) akikagua mitambo ya kuzalisha umeme katika kituo cha kufua umeme mkoani Kigoma.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu,( katikati) akiwapa maelekezo wasimamizi wa mitambo ya kufua umeme katika kituo cha kuzalisha a umeme mkoani Kigoma.

Watendaji wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu.( katikati) , alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi  katika kituo hicho.

…………………….

Na Zuena Msuya Kigoma,

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali inatarajia kuokoa takribani shilingi bilioni 25 zinazotumika kununua mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme katika Mkoa wa Kigoma kwa mwaka.

Akizungumza baada ya kutembelea kituo cha kuzalisha umeme mkoani Kigoma , Julai 12, Mgalu alisema serikali itaokoa fedha hizo, baada ya kuunganisha mkoa huo katika gridi ya taifa na kuacha kutumia umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta mazito.

Alisema kuwa tayari ujenzi njia ya kusafirisha umeme kuunganisha  Mkoa wa Kigoma katika gridi taifa umeanza ambapo itapita katika Wilaya ya Urambo mkoani  Tabora,Nguruka, na Kidawe mkoani Kigoma.

Vilevile aliweka wazi kuwa tayari ujenzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme katika njia hiyo ya kusafirisha umeme umeanza.

 “Serikali imekuwa ikitumia shilingi bilioni 25, kila mwaka kununua mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme Kigoma, lakini imekuwa ikiuuza umeme huo kwa shilingi bilioni 10 tu, hii ni hasara, hivyo tunatekeleza mpango mathubiti wa kumaliza changamoto hii”,alisema Mgalu.

Mradi huo ni wa kusafirisha umeme wa Kilovolti 132, na unatarajiwa kukamilika mwezi June 2020.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa huo,Mgalu alisema mkoa huo unahitaji umeme zaidi, ila kwa sasa upo mpango wa kuongeza mitambo ya kufua umeme katika wilaya zenye mahitaji  makubwa zaidi ikiwemo Wilaya ya Kasulu.

Mitambo hiyo ni ile iliyozimwa katika mikoa ambayo ilikuwa inatumia mafuta mazito kufua umeme , ambapo kwa sasa tayari imeunganishwa katika gridi ya taifa, na kuacha kutumia umeme unaozalishwa kwa  kutumia mafuta mazito.

Sambasamba na hilo, alitoa wito kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)kuwa, ujenzi wa njia ya umeme ukikamilika uende sambasamba na uimarishaji wa upatikanaji wa huduma ya umeme.

Pia kusitokee changamo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kwa lengo la kuwapatia huduma bora watumiaji katika kuendesha shughuli  za uzalishaji.

“ Tanesco katika mradi huu mjipange,mtimize azma ya serikali ya kuwapatia wananchi umeme wa kutosha na wa uhakika,wananchi wajue kweli wameingia kwenye gridi, siyo wanaingia kwenye gridi umeme unakatika hapana,nawapa tahadhari mapema,” alisisitiza Mgalu.

Akiuzungumzia fursa za Mkoa wa Kigoma, Mgalu amesema, serikali imedhamiria kuufanya Mkoa wa Kigoma kuwa  wenye viwanda na kuwavutia zaidi wawekezaji kwa kuwa mazingira yanaruhusu.