Home Mchanganyiko KILIMO CHA UMWAGILIAJI SULUHISHO LA MABADILIKO YA TABIANCHI

KILIMO CHA UMWAGILIAJI SULUHISHO LA MABADILIKO YA TABIANCHI

0

********

NA MWANDISHI MAALUM DODOMA

Kuwekeza katika kilimo cha Umwagiliaji kunaweza kuwa ni njia sahihi ya kuhimili
athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma
na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba
alipokuwa akifunga kongamano ya Wakulima lililoandaliwa na Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya
Umwagiliaji.

Mhandisi Futakamba alisema kuwa, Serikali imeweza kuwekeza kwa kiasi kikubwa
katika miundombinu ya Umwagiliaji na kuchukua jukumu kubwa la kutoa mafunzo
ya matunzo ya miundombinu hiyo kwa wakulima, ili kuweza kukabiliana na athari
na hasara zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi,

“ili kuweza kufikia lengo hili ni lazima serikali na wakulima kwenda pamoja ili kufanikisha, hali ambayo inaweza pia kusaidia wakulima nao kuingia zaidi katika kilimo cha biashara kama vile wakulima wa skimu ya Lemkuna na Pawaga, pamoja na kuwa na uhakika wa chakula nchini.” Alisema Mhandisi Mbogo.

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Marco
Ndonde alisema Tume hiyo imejipanga kuboresha Miundombinu ya kilimo cha
umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo benki ya kilimo na
mashirika mbalimbali ya maendeleo.

” Sambamba na hilo Tume ina mpango wa
kujenga mabwawa ili kufanya kilimo cha umwagiliaji kiwe na uhakika wa kupata
maji ya kutosha pamoja na kufungua miradi ya kilimo hicho kitakachoajiri vijana
kutoka vyuo vikuu nchini.” Alisisitiza Bw. Ndonde.

Akiwasilisha mada katika siku ya mwisho ya kongamano lililoshindanisha vyama
vya wamwagiliaji nchini, Bw. Fundi Mihayo kiongozi wa skimu ya umwagiliaji ya
Mkombilenga iliyopo Mkoani Iringa amesema, Lengo la Serikali kuwezesha
wakulima kuuza mchele badala ya kuuza mpunga katika maeneo ya skimu za
kilimo cha umwagiliaji limefanikiwa kwa kisia kikubwa kwani kwa sasa skimu
nyingi zimeweza kufunga mashine za kukoboa nafaka kama vile mpunga, na
kupaki katika madaraja na ujazo tofauti.

“Haya yote ni manufaa ya tokanayo na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania kutoa Mafunzo kwa kushirikiana na serikali ya Japan kupitia shirika lake
la JICA, jambo ambalo limepelekea wakulima kuwa na soko la uhakika la zao la
Mpunga hasa baada ya serikali kuhamia Makao makuu ya nchi Dodoma wakulima
wa skimu ya umwagiliaji Mkombilenga wamepata soko la uhakika Jijini Dodoma.”
Alisema Bw. Mihayo.

Wakitoa mawasilisho kwa baadhi ya skimu za umwagiliai zilizopo katika kanda
nane (8) za umwagiliaji nchini, wakulima wameonekana kutaja changamoto
mbalimbali wanazokabiliana nazo katika skimu hizo ikiwa ni pamoja na kuwepo
kwa hitaji la kuongeza mifereji inayopeleka maji katika skimu hizo pamoja na
kuisakafia na kuishauri Serikali kuendelea kutoa mafunzo kwa skimu zote ili
wakulima wapate uelewa na kutunza skimu jambo ambalo linaweza kusaidia
Serikali kufikia lengo la kuweza kuongeza kipato kwa wanachi na kuwepo kwa
uhakika wa chakula.

Skimu ya umwagilijai ya Mkombilenga iliyopo katika kanda ya Mbeya imeibuka
kidedea ikifuatiwa na skimu ya Lemkuna ya kanda ya Dodoma na skimu ya Nyida
iliyopo katika kanda ya Mwanza kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo.
Kongamano hilo la siku mbili lilishirikisha wakulima, wataalam wa kilimo toka
ngazi za Mikoa, Wilaya,Kanda za Umwagiliaji,Tamisemi na Ofisi za Tume ya
Umwagiliaji.