Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo,Prof. Mohammed Janabi akizungumzia hospitali hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda jinsi hospitali hiyo inavyofanya kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda akimuangalia mmoja wa watoto ambao wanaoendelea na matibabu baada ya kusumbuliwa na magonjwa ya moyo na kuwezam kufikishwa katika hospitali ya JKCCL kwaajili ya Matibabu.
***************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo Juni 22 ametimiza ahadi ya kutoa ufadhili wa matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto 10 kati ya 60 alioahidi kugharamia matibabu yao hadi pale watakapopona.
RC Makonda amesema ameamua kutoa ufadhili wa watoto 10 kila mwezi kwa kipindi cha miezi sita ambapo zoezi la upasuaji kwa watoto hao litaanza rasmi siku ya Jumatatu ya Juni24 kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea hundi ya Shilingi Milioni 10 kutoka taasisi ya Patel Samaj kwaajili ya matibabu ya watoto 10 kati ya 60 kutoka mikoa mbalimbali RC Makonda amesema walengwa ni watoto wanaotoka kwenye familia maskini ambazo zimepoteza matumaini kutokana na ukubwa wa garama za matibabu ambapo inaelezwa gharama ya upasuaji ni kwa mtoto mmoja ni kati ya Shilingi Milioni 8 hadi 10.
Aidha RC Makonda ameipongeza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa na nzuri ya kutoa huduma za kisasa kwa wagonjwa jambo lililosaidia kuokoa gharama zilizokuwa zikitumika kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.
Hata hivyo RC Makonda ameishukuru taasisi ya Patel Samaj kwa kumuunga mkono kupitia ufadhili matibabu kwa watoto hao ambapo ameziasa taasisi, makampuni na watu binafsi kusaidia matibabu kwa wenye uhitaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo,Prof. Mohammed Janabi amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa jitihada ambazo anazionyesha hasa baada ya kujitokeza na kuweza kusaidia watoto wwenye magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo kutibiwa
Aidha Prof. Janabi amemuomba Mkuu wa Mkoa aweze kuwapatia kiwanja ambacho kitaweza kuwasaidia kupata sehemu kubwa kwaajili ya huduma ambayo wanaitoa.
“Nimesikia unatoa viwanja, nakuomba uweze kutupatia eneo kubwa ambalo litaweza kurahisisha utoaji huduma hii kwani tunasehemu ndogo na tunawagonjwa wengi”. Amesema Prof.Janabi
Kwa upande wao wazazi wa watoto waliopata ufadhili huo kutoka mikoa mbalimbali wamemshukuru RC Makonda ambapo wameeleza kuwa kwa muda mrefu wamehangahika kutafuta pesa ya matibabu kwa watoto wao bila mafanikio kutokana na ukubwa wa garama.