SERIKALI mkoani Pwani ,imewaasa wenye viwanda kuhakikisha wanazalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya kisheria ya vipimo, ili kumlinda mteja,uchumi wa nchi na kupata tozo stahiki.
Aidha ,mamlaka za maji na jamii zimetakiwa kupeleka mita za maji kupima kwa wakala wa vipimo ili kuondoa malalamiko mbalimbali ikiwemo ubovu wa mita ama matumizi ya maji yasiyoendana na malipo .
Akitoa rai hiyo ,wakati alipotembelea mitambo ya kituo cha upimaji wa vipimo huko Misugusugu ,Kibaha,mkuu wa mkoa huo, Mhandisi Evarist Ndikilo
alieleza,yapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya viwanda wakiona wanabughudhiwa lakini ni lazima wazalishe bidhaa zinazoendana na vipimo.
“Viwanda vya saruji vizalishe saruji inayoendana na uzito sahihi na vipimo sahihi,nondo, na bidhaa zote zinazozalishwa viwandani ,kuliko kuwa na viwanda vingi vyenye bidhaa zisizo na viwango”alisisitiza Ndikilo.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa ,alisema mita za maji zimekuwa kero kwa watu wakidai wanaibiwa kuwa haziingiliani na vipimo.
“Mamlaka za maji na wananchi walio na kero hizo nendeni kwa wakala wa vipimo ili kuondoa kero hizo”alifafanua Ndikilo.
Awali ofisa mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo ,dkt Ludovick Manege alisema kituo hicho kinalenga kupima vimimina vya petrol,dizel na mita za maji.
Manege alibainisha kwamba, kwasasa wameunda kikosi maalum kwenda kukagua bidhaa viwandani kuangalia kama zinakidhi matakwa ya kisheria ya vipimo.